Ewe Nabii endelea hivyo hivyo, kama ulivyo, kumcha Mwenyezi Mungu, wala usiyakubali mawazo ya makafiri na wanaafiki. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa kuvijua, ni Mwenye hikima katika kauli yake na vitendo vyake.
Na fuata wahyi unao teremka juu yako kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu anaye kufunulia kwa wahyi anazo khabari hata za mambo madogo madogo unayo yatenda wewe, na wanayo yatenda makafiri na wanaafiki.
Mwenyezi Mungu hakumjaalia mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake; wala hakumfanya mke wa yeyote katika nyinyi kuwa ni mama yake, pale anapo sema ati: Wewe kwangu mimi kama mgongo wa mama yangu! Wala hakuwafanya watoto mnao wapanga kuwa ni wenenu, kuwa hakika ni wana wenu kwa nasaba. Hayo ya kuwafanya watoto wa kupanga kuwa ni wenenu, ni kauli inayo toka kwenye vinywa vyenu, wala hayana ukweli. Hapana hukumu yoyote inayo tokana na hayo. Na Mwenyezi Mungu anasema jambo lilio thibiti la hakika. Na anakuongozeni mlifikie. Na Yeye peke yake Subhanahu ndiye anaye ongoa watu kwenye Njia iliyo sawa.
Wanasibishieni hawa watoto kwa baba zao khasa. Hayo ndiyo ya uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Ikiwa hamwajui baba zao walio nasibiana nao khasa, basi hao ni ndugu zenu katika Dini na rafiki zenu wa kuwanusuru. Wala nyinyi hamna dhambi ikiwa mmewanasibisha na watu wasio kuwa baba zao kwa kukosea. Lakini inakuwa dhambi kwa mlio kusudia kwa nyoyo zenu baada ya kwisha jua yaliyo. Na Mwenyezi Mungu anakusameheni kwa kukosea kwenu, na anaikubali toba yenu kwa makosa mliyo kusudia.
Nabii Muhammad ni mwenye kustahiki zaidi urafiki kwa Waumini, na ana huruma zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Basi yawapasa wao wampende na wamt'ii. Na wake zake ni Mama zao kwa kuwatukuza na kuwahishimu, na kuwa ni haramu juu yao kuwaoa baada yake. Na jamaa walio khusiana ni karibu zaidi kuliko Waumini wenginewe na Wahajiri, walio hama Makka, kwa kurithiana wao kwa wao kama ilivyo wajibika katika Qur'ani. Lakini inafaa kumfanyia wema mlio fanya urafiki naye katika Dini asiye kuwa jamaa yenu, kwa kuwapa wema na mapenzi au hata kumuandikia mali katika wasia. Hayo ya kurithiana jamaa walio khusiana yamethibiti katika Kitabu cha Qur'ani wala hayawezi kubadilishwa.