Hapana wa kuwalipa kwa vitendo vyao na kazi zao ila Mola wangu Mlezi; kwani Yeye ndiye anaye yajua vyema ya undani wao. Kama nyinyi ni watu watambuzi mngeli tambua hayo.
Mimi si chochote ila ni Mtume niliye toka kwa Mwenyezi Mungu kuwaonya walio wajibikiwa kwa onyo lilio wazi, kwa ushahidi wa kutenganisha baina ya kweli na uwongo, bila ya farka yoyote baina ya mtukufu na mnyonge. Basi vipi itanifalia mimi kuwafukuza Waumini kwa sababu ya ufakiri wao?
Basi tuhukumie baina yangu na wao, kwa hukumu ya kuwaangamiza wanao pinga Upweke wako, na wakamkadhibisha Mtume wako! Na niokoe mimi na Waumini walio pamoja nami na adhabu ya uasi wao.
Hakika katika yaliyo simuliwa na Qur'ani juu ya khabari za Nuhu ni hoja ya kuthibitisha ukweli wa Mitume na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na katika watu walio somewa hadithi hizi si wengi walio amini.
Wala kwa hii nasaha yangu na uwongozi wangu sitaki kwenu ujira. Sina malipo isipo kuwa kwa Muumba wa viumbe vyote.
Je! Mnasimamisha juu ya kila pahala palipo nyanyuka katika nchi jengo refu kwa ajili ya kujifakhirisha, na mnakutana humo kwa mambo ya upuuzi na fisadi? Mwenyezi Mungu Subhanahu anataka kwa haya kuwazindua watende yatakayo wanufaisha, na anawatahayarisha kwa kuacha kwao Imani na vitendo vyema.
Mimi nina khofu asije Mwenyezi Mungu akakuteremshieni adhabu kali hapa duniani, na Akhera akakutieni katika Moto wa Jahannamu kwa sababu ya ujabari wenu na starehe alizo kustarehesheni Mwenyezi Mungu.