Qurani Kərimin mənaca tərcüməsi - Səvahili dilinə tərcümə - Əli Muhsin əl-Bərvani.

Səhifənin rəqəmi:close

external-link copy
220 : 2

فِي ٱلدُّنۡيَا وَٱلۡأٓخِرَةِۗ وَيَسۡـَٔلُونَكَ عَنِ ٱلۡيَتَٰمَىٰۖ قُلۡ إِصۡلَاحٞ لَّهُمۡ خَيۡرٞۖ وَإِن تُخَالِطُوهُمۡ فَإِخۡوَٰنُكُمۡۚ وَٱللَّهُ يَعۡلَمُ ٱلۡمُفۡسِدَ مِنَ ٱلۡمُصۡلِحِۚ وَلَوۡ شَآءَ ٱللَّهُ لَأَعۡنَتَكُمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٞ

--Katika mambo ya dunia na mambo ya Akhera. Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu; na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Mwenyezi Mungu angeli penda angeli kutieni katika udhia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima. info

Na wanakuuliza khabari ya mayatima: katika Uislamu inapasa watendejwe? Sema ni kheri yenu na yao kuwatendea wema. Wawekeni katika nyumba zenu pamoja nanyi, na changanyikeni nao kwa makusudio ya kheri si ya fisadi, kwani wao ni ndugu zenu duniani, wanahitaji kwenu mchanganyiko huu. Na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji katika nyinyi. Basi tahadharini! Na Mwenyezi Mungu angeli penda angeli kupeni taabu, akakulazimisheni kuwaangalia mayatima bila ya kuchanganyika nao, au angeli kuacheni bila ya kubainisha waajibu wanao pasa kutendewa. Kwa hivyo wangeli kulia kuchukia watu, na hayo yange pelekea kufisidika na kuleta shida kwa jamii zenu. Kwani kuwakahirisha mayatima na kuwadhili huwafanya wawachukie hao jamaa wawatendao vibaya. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda katika amri yake, lakini naye ni Mwenye hikima halazimishi katika sharia ila lenye maslaha yenu.

التفاسير:

external-link copy
221 : 2

وَلَا تَنكِحُواْ ٱلۡمُشۡرِكَٰتِ حَتَّىٰ يُؤۡمِنَّۚ وَلَأَمَةٞ مُّؤۡمِنَةٌ خَيۡرٞ مِّن مُّشۡرِكَةٖ وَلَوۡ أَعۡجَبَتۡكُمۡۗ وَلَا تُنكِحُواْ ٱلۡمُشۡرِكِينَ حَتَّىٰ يُؤۡمِنُواْۚ وَلَعَبۡدٞ مُّؤۡمِنٌ خَيۡرٞ مِّن مُّشۡرِكٖ وَلَوۡ أَعۡجَبَكُمۡۗ أُوْلَٰٓئِكَ يَدۡعُونَ إِلَى ٱلنَّارِۖ وَٱللَّهُ يَدۡعُوٓاْ إِلَى ٱلۡجَنَّةِ وَٱلۡمَغۡفِرَةِ بِإِذۡنِهِۦۖ وَيُبَيِّنُ ءَايَٰتِهِۦ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمۡ يَتَذَكَّرُونَ

Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini yake. Naye huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate kukumbuka. info

Hapana ubaya wowote kuchanganyika na mayatima, lakini kuchanganyika na washirikina ni vibaya. Muumini hana ruhusa kumwoa mshirikina asiye fuata dini ya Kitabu cha mbinguni. Basi msipelekewe kutaka kumwoa mwanamke wa kishirikina kwa ajili ya mali yake, au uzuri wake, au jaha yake, au ukoo wake. Muumini aliye mtumwa ni bora kuliko mshirikina aliye huru mwenye mali, na jamali, na utukufu na nasaba. Wala nyinyi msiwaoeze wanawake walio mikononi mwenu wanaume wa kishirikina wasio amini Vitabu vya mbinguni, wala yasikupelekeeni kumkhiari mshirikina utajiri na cheo chake. Mtumwa Muumini ni bora kuliko huyo. Hao washirikina wanawavutia wenzao kwenda katika maasi na ushirikina, na kwa hivyo wanapaswa kuingia Motoni. Na Mwenyezi Mungu anapo kulinganieni mjitenge na ndoa za washirikina anakulinganieni kwa ajili ya maslaha yenu na mwongoke ili mpate Pepo na maghfira, na mwende katika njia ya kheri kwa taisiri. Na Mwenyezi Mungu anabainisha sharia zake na uwongofu wake kwa watu wapate kujua maslaha yao na kheri yao.

التفاسير:

external-link copy
222 : 2

وَيَسۡـَٔلُونَكَ عَنِ ٱلۡمَحِيضِۖ قُلۡ هُوَ أَذٗى فَٱعۡتَزِلُواْ ٱلنِّسَآءَ فِي ٱلۡمَحِيضِ وَلَا تَقۡرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطۡهُرۡنَۖ فَإِذَا تَطَهَّرۡنَ فَأۡتُوهُنَّ مِنۡ حَيۡثُ أَمَرَكُمُ ٱللَّهُۚ إِنَّ ٱللَّهَ يُحِبُّ ٱلتَّوَّٰبِينَ وَيُحِبُّ ٱلۡمُتَطَهِّرِينَ

Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wat'ahirike. Wakisha t'ahirika basi waendeeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha. info

Na wanakuuliza juu ya kuwaingilia wake zenu wakati wanapo kuwa na damu ya mwezi, hedhi. Waambie kuwa hedhi ni uchafu. Basi jizuieni kuwaingilia wakati wake mpaka wat'ahirike (wasafike). Wakit'ahirika basi ingianeni nao katika njia za maumbile. Na ikiwa mtu amefanya makosa katika haya, basi na atubu, na Mwenyezi Mungu anapenda waja wake wakithiri toba na usafi kutokana na uchafu. Ilimu ya kisasa zimethibitisha kuwa wakati wa hedhi yanaweza kuwa madhara kwa kuwa zalio huweza kupata maradhi pindi likiingiliwa na vidudu vya maradhi, ambavyo ni vyepesi kuingia wakati wa kuingiliana na mwanamume. Maradhi hayo huenda yakasababisha mwanamke asiweze kuzaa. Mwanamume naye huambukia maradhi hayo kutokana na mwanamke kwa kupitia njia za mkojo, na maradhi yakapanda juu mpaka mafigo yakaharibika, na kuathirika vyombo vya uzazi, na mwanamume naye akawa hawezi kutia mimba. Maradhi haya huleta machungu makubwa. Watu walikuwa hawajui, lakini Mwenyezi Mungu anajua kila kitu. Na mwanamke anapo kuwa na damu anakuwa hana raghba ya kuingiliwa, basi kumuingilia wakati huo huenda kukamletea hali ya nafsi mbaya na chuki kwa jambo hilo.

التفاسير:

external-link copy
223 : 2

نِسَآؤُكُمۡ حَرۡثٞ لَّكُمۡ فَأۡتُواْ حَرۡثَكُمۡ أَنَّىٰ شِئۡتُمۡۖ وَقَدِّمُواْ لِأَنفُسِكُمۡۚ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّكُم مُّلَٰقُوهُۗ وَبَشِّرِ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ

Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara njema Waumini. info

Wake zenu ni mwahali mwa kupatia uzazi, kama vile mbegu inavyo toa mmea. Basi ni halali kwenu kuwaingilia vyovyote kwa sharti ya kupitia njia za uzazi. Na mcheni Mwenyezi Mungu wala msimuasi katika kukaa kwenu na wanawake. Na mjue kuwa nyinyi mtakutana naye, na mna jukumu kwake. Furaha ni ya hao wanao simama juu ya mipaka yake Mtukufu na hawaikiuki.

التفاسير:

external-link copy
224 : 2

وَلَا تَجۡعَلُواْ ٱللَّهَ عُرۡضَةٗ لِّأَيۡمَٰنِكُمۡ أَن تَبَرُّواْ وَتَتَّقُواْ وَتُصۡلِحُواْ بَيۡنَ ٱلنَّاسِۚ وَٱللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٞ

Wala msifanye jina la Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu kuwa ni kisingizio cha kuacha kufanya wema na kuchamngu na kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua. info

Msilichezee jina la Mwenyezi Mungu katika kukithirisha viapo, kwani hivyo inakuwa ni kinyume na kulitukuza jina la Mwenyezi Mungu. Na hakika kujilinda na kukithirisha kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ndio hupelekea vitendo vyema, na kuchamngu, na kuweza kusuluhisha baina ya watu. Mwenye kujilinda hivyo huwa anatukuka cheo katika macho ya watu, na anakuwa anaaminika, na kauli yake hukubalika kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno yenu na yamini zenu, na Mjuzi wa niya zenu.

التفاسير: