Ikiwa hao maadui wanataka kukukhadaa na kukufanyia ujanja kwa hivyo kuonyesha kuwa wanataka amani, basi Mwenyezi Mungu anakutosheleza kukulinda na vitimbi vyao kwa kila upande. Kwani Yeye alikwisha tangulia kukuunga mkono kwa kukupa ushindi pale alipo kutengenezea sababu zilizo onekana na za siri za kutia imara nyoyo za Waumini katika Wahajiri, wahamiaji walio toka Makka, na Ansari, wasaidizi wa Madina.
Na Mwenyezi Mungu akawaweka pamoja kwa mapenzi baada ya mtafaruku na uadui, hata wakawa marafiki mbele yako, wakizisabilia roho zao na mali yao kwa ajili ya wito wako. Na wewe hata ungeli toa mali yote na vitu vyote vya nafuu viliomo duniani kwa ajili ya kuwaunga pamoja huku, usinge weza kuyapata hayo. Kwa sababu nyoyo zimo katika mkono wa Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye aliye waunganisha, kwa kuwaongoa kwenye Imani na mapenzi na udugu. Hakika Yeye Mtukufu ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda. Anawapangia waja wake kwa mujibu wa manufaa yao.
Ewe Nabii! Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kukudhamini wewe na wenye kukufuata miongoni mwa Waumini katika kila jambo lenye maana kwenu.
Ewe Nabii! Wahimize Waumini wende vitani kwa ajili ya kulinyanyua Neno la Mwenyezi Mungu, na wapendezeshe kwa yatayo wafwatia katika kheri ya dunia na Akhera watayo ipata, ili nafsi zao ziingie nguvu. Nayo ikiwa wapo kati yenu watu ishirini walio shikamana na Imani na subira na ut'iifu, basi watawashinda makafiri mia mbili. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio fahamu ukweli wa mambo, kwani hawana Imani, wala subira, wala tamaa ya kupata thawabu.
Ilivyo kuwa ni waajibu wenu enyi Waumini, kusubiri mnapo kutana na maadui zenu katika hali ya kuwa mna nguvu, ijapo kuwa wamekuzidini mara kumi, sasa Mwenyezi Mungu amekuruhusini katika hali isiyo kuwa ya nguvu, kuwa mvumilie ikiwa adui kakuzidini mara mbili basi. Hayo ni kwa kukujua kwake kuwa hamna nguvu nyingi, kwa hivyo mmefanyiwa wepesi na mmesahilishiwa, baada ya kuwa heba ya Uislamu imeingia katika nafsi za makafiri. Kwa hivyo mkiwa nyinyi ni wapiganaji mia wenye kusubiri mnaweza kuwashinda makafiri mia mbili. Na mkiwa elfu moja mtawashinda elfu mbili, kwa Mwenyezi Mungu kupenda na kusaidia. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri kwa nusura yake na kuunga mkono kwake.
Haimfalii Nabii yeyote kukamata mateka, au kuchukua fidia, au kutoa bure msamaha, mpaka ashinde, na maadui waone wameshindwa, na wawe wamepata pigo kubwa hata kuwa hawawezi tena kupigana katika nchi. Lakini, nyinyi jamaa wa Kiislamu, mmefanya haraka katika Vita vya Badri kukamata mateka kabla hamjatamakani mkawa imara katika nchi. Mnatafuta manufaa ya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera, kwa kutukuzwa Neno la Haki, na lisikushughulisheni la dunia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda. Hukupangieni mambo yenu kwa mujibu wa faida yenu.
Ingeli kuwa hapana hukumu iliyo kwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kumsamehe mwenye kujitahidi japo kuwa amekosa, basi ingeli kupateni adhabu kubwa kwa papara mliyo ifanya.
Basi sasa tumieni mlicho kipata katika fidia kwa kuwa ni halali kwenu, wala si uchumi muovu. Na mcheni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote. Hakika Mwenyezi Mungu ni mkubwa wa kusamehe na kumrehemu amtakaye katika waja wake pindi akirejea.