Ilivyo kuwa ni waajibu wenu enyi Waumini, kusubiri mnapo kutana na maadui zenu katika hali ya kuwa mna nguvu, ijapo kuwa wamekuzidini mara kumi, sasa Mwenyezi Mungu amekuruhusini katika hali isiyo kuwa ya nguvu, kuwa mvumilie ikiwa adui kakuzidini mara mbili basi. Hayo ni kwa kukujua kwake kuwa hamna nguvu nyingi, kwa hivyo mmefanyiwa wepesi na mmesahilishiwa, baada ya kuwa heba ya Uislamu imeingia katika nafsi za makafiri. Kwa hivyo mkiwa nyinyi ni wapiganaji mia wenye kusubiri mnaweza kuwashinda makafiri mia mbili. Na mkiwa elfu moja mtawashinda elfu mbili, kwa Mwenyezi Mungu kupenda na kusaidia. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri kwa nusura yake na kuunga mkono kwake.