আল-কোৰআনুল কাৰীমৰ অৰ্থানুবাদ - শ্বাহিলি অনুবাদ- আলী মুহছিন আল-বাৰওৱানী

পৃষ্ঠা নং:close

external-link copy
53 : 8

ذَٰلِكَ بِأَنَّ ٱللَّهَ لَمۡ يَكُ مُغَيِّرٗا نِّعۡمَةً أَنۡعَمَهَا عَلَىٰ قَوۡمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُواْ مَا بِأَنفُسِهِمۡ وَأَنَّ ٱللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٞ

Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizo waneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika Mwwnyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. info

Na huu ni uadilifu katika kulipa, kwa sababu Mwenyezi Mungu hakika haibadilishi neema anayo waneemesha watu, kama vile neema ya amani, kutononoka, na afya, mpaka wao wenyewe waigeuze hali yao na sababu zake! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia wayasemayo, na Mwenye kuyajua wayatendayo.

التفاسير:

external-link copy
54 : 8

كَدَأۡبِ ءَالِ فِرۡعَوۡنَ وَٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِهِمۡۚ كَذَّبُواْ بِـَٔايَٰتِ رَبِّهِمۡ فَأَهۡلَكۡنَٰهُم بِذُنُوبِهِمۡ وَأَغۡرَقۡنَآ ءَالَ فِرۡعَوۡنَۚ وَكُلّٞ كَانُواْ ظَٰلِمِينَ

Ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao - walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, basi tukawateketeza kwa madhambi yao. Na tukawazamisha watu wa Firauni. Na wote walikuwa wenye kudhulumu. info

Kama ilivyo kuwa ada yao na mtindo wao hawa katika kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na neema zake ni kama mtindo wa watu wa Firauni na walio watangulia, hali kadhaalika ada yao na shani yao katika kuendelea kuwakadhibisha Mitume wake, na dalili za Unabii wao, ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao. Basi wamefanana hao katika kukanusha Ishara, na kuupinga Utume wa Mitume, na kuwakadhibisha, na kuendelea juu ya mwendo huo vile vile. Na kila mmoja Mwenyezi Mungu amemtia mkononi kwa dhambi zake -wale kwa midharuba, na vimbunga, na kadhaalika; na watu wa Firauni kwa kuwazamisha. Na wote walikuwa ni madhaalimu wa nafsi zao. Kwa hivyo walistahiki adhabu iliyo wafika.

التفاسير:

external-link copy
55 : 8

إِنَّ شَرَّ ٱلدَّوَآبِّ عِندَ ٱللَّهِ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ فَهُمۡ لَا يُؤۡمِنُونَ

Hakika vinyama vilio viovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao kufuru, basi hao hawaamini; info

Hakika katika vyote vilio enea juu ya uso wa ardhi walio waovu mno mbele ya Mwenyezi Mungu katika hukumu yake na uadilifu wake, ni makafiri walio kakamia juu ya ukafiri wao,

التفاسير:

external-link copy
56 : 8

ٱلَّذِينَ عَٰهَدتَّ مِنۡهُمۡ ثُمَّ يَنقُضُونَ عَهۡدَهُمۡ فِي كُلِّ مَرَّةٖ وَهُمۡ لَا يَتَّقُونَ

Wale ambao miongoni mwao umepatana nao ahadi, kisha wanavunja ahadi yao kila mara, wala hawamchi Mungu. info

Nao ni wale ulio fungamana nao kwa mikataba, nao wakawa hawaachi kuivunja kila mara; na watu hao ni Mayahudi ambao hawachelei utukufu wa Mwenyezi Mungu, wala hawakhofu kupatilizwa naye, wala adhabu yake.

التفاسير:

external-link copy
57 : 8

فَإِمَّا تَثۡقَفَنَّهُمۡ فِي ٱلۡحَرۡبِ فَشَرِّدۡ بِهِم مَّنۡ خَلۡفَهُمۡ لَعَلَّهُمۡ يَذَّكَّرُونَ

Basi ukiwakuta vitani wakimbize walio nyuma yao ili wapate kukumbuka. info

Basi ewe Mtume! Ukiwakuta hawa wavunjao mapatano, na ukasadifiana nao katika vita nawe umeshinda, basi watishe baraabara kwa kuwapa adhabu ya kuwatia uchungu na kuwaogopesha wale walio nyuma yao, upate kuwafarikisha walio baki. Mateso haya ndiyo ya kuwakumbusha uovu wa kuvunja mapatano, na kuwazuia wenginewe wasitende kama hayo. Katika Aya tukufu hizi tunahadharishwa na wale wanao toa ahadi na kisha wakazivunja. Hawa yafaa wapewe adhabu ya kutia mfano kwao na kwa walio nyuma yao. Na katika Aya hii unabainishwa umuhimu wa kuvuruga askari wa adui walio nyuma. Hizi ni mbinu za vita za kisasa, kwani kuzua vurugo katika askari wa nyuma hutosha kuleta fujo na kupelekea jeshi kutawanya askari wake kulinda mgongo wake, na kwa hivyo zinavunjika nguvu zake. Juu ya hivyo katika sehemu za nyuma katika midani ndio huwapo mambo yaliyo khusu idara ya jeshi ambayo juu yake ndio jeshi linategemea kwa msaada. Ukileta vurugu hapa hupelekea kukosekana nidhamu yote ya jeshi, na kwa hivyo ndio huleta kuemewa na kushindwa.

التفاسير:

external-link copy
58 : 8

وَإِمَّا تَخَافَنَّ مِن قَوۡمٍ خِيَانَةٗ فَٱنۢبِذۡ إِلَيۡهِمۡ عَلَىٰ سَوَآءٍۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُحِبُّ ٱلۡخَآئِنِينَ

Na ukichelea khiana kwa watu fulani basi watupilie ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini. info

Na ukiona alama za hao watu kutaka kuleta khiana kuvunja maagano yaliyo baina yako na wao, ikate njia yao wasiweze kukukhuni, kwa kuwatangazia wewe kuvunja hayo mapatano, mpaka walijue jambo lako, na wasiweze kukukhuni. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini, wala haridhii kuwa nyinyi msifike kwa sifa yao.

التفاسير:

external-link copy
59 : 8

وَلَا يَحۡسَبَنَّ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ سَبَقُوٓاْۚ إِنَّهُمۡ لَا يُعۡجِزُونَ

Wala wasidhanie wale walio kufuru kwamba wao wametangulia mbele. La, wao hawatashinda. info

Wala wasidhani walio kufuru kuwa wamekwisha tangulia na wameiepuka adhabu ya kukhuni kwao na kwenda kinyume! Wao kabisa hawatamshinda Mwenyezi Mungu asiwazunguke na kuwatia nguvuni, bali Yeye peke yake ni Muweza, na atawalipa kwa nguvu zake na uadilifu wake.

التفاسير:

external-link copy
60 : 8

وَأَعِدُّواْ لَهُم مَّا ٱسۡتَطَعۡتُم مِّن قُوَّةٖ وَمِن رِّبَاطِ ٱلۡخَيۡلِ تُرۡهِبُونَ بِهِۦ عَدُوَّ ٱللَّهِ وَعَدُوَّكُمۡ وَءَاخَرِينَ مِن دُونِهِمۡ لَا تَعۡلَمُونَهُمُ ٱللَّهُ يَعۡلَمُهُمۡۚ وَمَا تُنفِقُواْ مِن شَيۡءٖ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ يُوَفَّ إِلَيۡكُمۡ وَأَنتُمۡ لَا تُظۡلَمُونَ

Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu, na wengineo ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa. info

Enyi Umma wa Kiislamu! Tayarisheni kila muwezavyo nguvu za vita za namna zote kwa ajili ya kujizatiti kwa ajili ya kupigana, na wekeni askari walinzi na farasi wao mipakani na kando kando ya nchi, ili kwa hivi mjitayarishe na ulinzi mwatie kiwewe adui za Mwenyezi Mungu na adui zenu miongoni mwa hao makafiri ambao wamo kungojea likupateni jambo. Na pia mpate kuwatishia wenginewe ambao nyinyi hamwajui hivi sasa, lakini Mwenyezi Mungu anawajua, kwani hapana jambo linalo jificha kwake. Na kila mnacho kitoa kwa kuzitayarisha nguvu zenu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi Yeye atakulipeni malipo ya kutosha, bila ya kupunguka hata chembe katika mnayo stahiki katika fadhila ya Mola wenu Mlezi Katika Aya hii tukufu pana kuhimizwa na kuamrishwa kujitayarisha kwa ajili ya kupambana na adui. Kwani vita, zamani na sasa, ni jambo la khatari na muhimu kabisa. Juu yake inategemea kheri na shari, kufa kupona kwa umati na umati. Basi yapasa kujitayarisha, kujizatiti, na kujitengeneza kwa jiha mbali mbali za vifaa na silaha na zana. Kuingia vitani bila ya kujipatia zana zote na kujitayarisha ni kutafuta kushindwa. Na tunaona hivi sasa madola yanavyo jiandaa wakati wa amani na vita, na yanavyo jenga siasa zao na mipango yao na wanavyo kusanya uwezekano wao wote ili wapate ushindi katika vita. Na vita sasa havimsazi mtu. Wanashiriki katika vita wanajeshi na raia. Kwa hivyo ndio inapasa zaidi kujitengeneza kila mmoja wao kwa matengenezo ya kuwakusanya na kuwaweka tayari wote ili upatikane ushindi.

التفاسير:

external-link copy
61 : 8

۞ وَإِن جَنَحُواْ لِلسَّلۡمِ فَٱجۡنَحۡ لَهَا وَتَوَكَّلۡ عَلَى ٱللَّهِۚ إِنَّهُۥ هُوَ ٱلسَّمِيعُ ٱلۡعَلِيمُ

Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. info

Maadui wakielekea kutaka amani na kuacha uadui wao, basi nawe ewe Mtume, elekea kwenye amani. Kwani vita sio lengo, bali wewe unakusudia kujilinda tu na uadui wao na upinzani wao kupinga wito wako. Basi kubali amani, na umtegemee Mwenyezi Mungu, wala usikhofu vitimbi vyao na njama zao! Yeye Subhanahu ni Mwenye kuzisikia njama zao, ni Mwenye kuijua mipango yao. Hapana kinacho fichikana kwake. Huu ni msingi mkuu katika misingi ya Uislamu, Dini ya Salama. Na leo tunasikia kila dola duniani ina nadi Usalama, na kwa hivyo ukaundwa Umoja wa Mataifa.

التفاسير: