Hao makafiri hawana nguvu za kumshinda Mwenyezi Mungu asiwatie nguvuni duniani akawaadhibu; na hawana wasaidizi wa kuweza kuwakinga na adhabu yake pindi Mwenyezi Mungu akitaka kuwaletea hiyo katika Akhera, hata ikiwa mardufu ya ile ambayo wangeli ipata duniani, ingeli kuwa Mwenyezi Mungu anataka iwafikie. Kwa sababu hao wamechukia kuisikia Qur'ani, na kuzingatia Ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu. Wamekuwa kama kwamba hawakuwa wakiweza kusikia wala kuona.
Hao makafiri hawapati faida yoyote katika kumuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu! Bali wamejikhasiri nafsi zao, na huko Akhera huo uwongo walio kuwa wakiuzua, na madai ya upotovu, na miungu ya uwongo waliyo kuwa wakiiunda, na wakadai kuwa hiyo ati ikiwafaa au itawaombea - yote hayo yatawapotea. Kwa sababu hakika Siku ya Kiyama ndiyo Siku ya hakika, ambayo haina udanganyifu wala uzushi.
Bila ya shaka wale wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wakatenda a'mali njema, na nyoyo zao zikanyenyekea na zikatua kuikubali hukumu ya Mola wao Mlezi, hao ndio wanao stahiki kuingia Peponi na kudumu humo milele.
Mfano wa makundi mawili hayo, ya Waumini na makafiri, ni kama kipofu anaye kwenda bila ya uwongofu na kiziwi asiye sikia uwongozi wa kuokoka, na kundi la pili ni kama mwenye macho anaye iona njia ya kheri na uokofu, na mwenye masikio makali anaye sikia kila lenye manufaa naye. Makundi mawili hayo hayawezi kuwa sawa katika hali yao na kuishia kwao! Basi, enyi watu, hamfikiri yaliyo baina yenu ya khitilafu ya utambuzi na ukafiri, na khitilafu baina ya baat'ili na Haki, mkawa mbali na njia ya upotovu, na mkaishika Njia Iliyo Nyooka?
Na kama tulivyo kutuma kwa watu wako uwaonye na uwabashirie kheri, wakakukabili baadhi yao kwa inadi na upinzani, kadhaalika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akawaambia: Mimi nakuhadharisheni na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na nakuonyesheni njia ya kuokoka.
Akawaambia: Mimi nilitakalo kwenu ni kuwa msimuabudu ila Mwenyezi Mungu tu, kwa sababu nakukhofieni, mkimuabudu mwenginewe au mkimshirikisha pamoja naye wenginewe katika kumuabudu, isije ikakufikieni siku ya adhabu yake yenye machungu makali.
Wakuu wa kaumu yake wakasema: Sisi hatukuoni wewe ila kuwa ni mtu kama sisi. Hapana lolote linalo kufanya uwe namna ya peke yako, au uwe na ubora wa kutupelekea tukuamini kuwa wewe ni Mtume utokaye kwa Mwenyezi Mungu! Na wala hatuwaoni hao walio kufuata ila ni watu wa t'abaka la chini miongoni mwetu! Wala hatukuoneni nyinyi kuwa ni bora kuliko sisi! Bali sisi tunaitakidi kuwa nyinyi ni waongo tu katika hayo mnayo dai.
Nuhu akasema: Enyi watu! Hebu nambieni, ikiwa mimi naungwa mkono na hoja zilizo wazi kutokana na Mola wangu Mlezi, naye akanipa kwa rehema yake Unabii na Utume, na nuru yake ikafichikana kwenu, na kughurika kwenu kwa cheo na mali kukakutieni upofu msizione, basi je, itafaa tukulazimisheni mziamini hoja kwa nguvu na karaha?