Zilipo dhihiri Aya (Ishara) za Qur'ani kutokana na Mtume wetu Muhammad juu ya washirikina, walisema makafiri wasio ikhofu adhabu ya Mwenyezi Mungu wala hawataraji thawabu zake: Tuletee kitabu kinginecho kisicho kuwa hii Qur'ani. Au badilisha yaliyomo humu, yale yasiyo tupendeza. Waambie ewe Mtume: Hayumkini wala haijuzu mimi kugeuza au kubadilisha kwa nafsi yangu. Mimi si chochote ila ni mwenye kufuata na mwenye kufikisha kile kinacho funuliwa kwangu kutokana na Mola wangu Mlezi. Mimi naogopa, nikienda kinyume na Wahyi, Ufunuo, wa Mola wangu Mlezi, adhabu ya Siku ambayo khatari yake ni kuu, na kitisho chake ni kikubwa!
Waambie ewe Mtume! Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa asiniteremshie Qur'ani kutoka kwake, wala mimi nisikufikishieni, asingeli teremsha, wala mimi nisingeli kusomeeni, na wala Mwenyezi Mungu asingeli kufundisheni. Lakini Yeye kateremsha, na kanituma mimi kwayo, na mimi nimekusomeeni kama alivyo niamrisha. Na mimi nilikwisha kaa nanyi wakati mrefu kabla ya kupewa Utume, na mimi sikudai Utume wakati huo, wala sikukusomeeni kitu chochote. Na nyinyi mmeshuhudia kuwa mimi ni mkweli na muaminifu. Lakini umekuja Ufunuo na nimeamrishwa niusome. Basi hebu yatieni akilini haya mambo, na myazingatie, na yakutanisheni yaliyo pita ya zamani na ya yaliopo sasa.
Hapana mtu aliye jidhulumu nafsi zaidi kuliko anaye kufuru na akamzulia uwongo Mwenyezi Mungu, au akazikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu alizo kuja nazo Mtume wake. Hakika hafuzu kafiri katika vitendo vyake. Naye amekhasiri khasara iliyo wazi kwa ukafiri wake na amemghadhibisha Mwenyezi Mungu.
Na hawa washirikina wanao mzulia Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika, wanaabudu masanamu ya upotovu. Hayawadhuru wala hayawanufaishi. Na wanasema: Masanamu haya yatatuombea kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Akhera! Ewe Mtume! Waambie: Hivyo nyinyi mnamwambia Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika ambao hawajui, la katika mbingu wala katika ardhi? Mwenyezi Mungu ametakasika na kuwa na washirika, na yote mnayo zua kwa kuwaabudu hao washirika.
Watu kwa maumbile yao hawakuwa ila ni Umma mmoja tu. Kisha tukawapelekea Mitume wawaongoze na wawaongoe kwa mujibu wa Ufunuo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ikawa tabia ya kibinaadamu iliyo pelekea kheri na shari ndiyo sababu ya kuwa na nguvu zaidi shari katika baadhi yao. Juu yao hao matamanio na nyendo za Shetani zikatawala, na kwa hivyo wakakhitalifiana. Na lau kuwa hukumu ya Mola wako Mlezi haikutangulia ya kuwapa muhula makafiri kwa ajili yako, Ewe Nabii, na kuakhirisha maangamizo yao mpaka siku maalumu iliyo ahidiwa, Mwenyezi Mungu angeli wapelekea upesi maangamizo na adhabu, kwa sababu ya mfarakano waliyo uingia, kama zilivyo ingia kaumu zilizo kwisha pita.
Na hawa washirikina wanasema: Hivyo Muhammad hateremshiwi muujiza usio kuwa hii Qur'ani, wa kutuyakinisha Utume wake? Waambie Ewe Mtume! Kuteremshwa Ishara ni jambo la ghaibu, hapana alijuaye ila Mwenyezi Mungu. Kama Qur'ani haikufaini basi ngojeni hukumu ya Mwenyezi Mungu baina yangu na nyinyi katika hayo mnayo yabisha. Na mimi ni pamoja nanyi katika wanao ngojea.