Yanayo kupata kutoka kwa watu wako, yaliwapata Manabii walio kutangulia. Basi wasomee hawa watu, Ewe Mtume, aliyo kuteremshia Mola wako Mlezi katika Qur'ani kisa cha Nuhu, Mtume wa Mwenyezi Mungu. Alipo iona chuki na uadui wa watu wake kwa ujumbe wake, aliwaambia: Enyi watu wangu! Ikiwa kuwa pamoja nanyi kwa ajili ya kufikisha ujumbe kumekuwa ni shida juu yenu, basi mimi ni mwenye kuendelea na wito wangu, na ni mwenye kushikilia hapo hapo, na ni mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu katika hili jambo langu. Basi nyinyi na washirika wenu jifungeni madhubuti katika shauri yenu, wala msiufiche uadui wenu kwangu kabisa, wala msinipe muhula wowote kwa maovu mnayo nipangia kunitendea, kama kweli mnaweza kuniletea madhara. Kwani Mola wangu Mlezi ananilinda.
Na ikiwa mtabaki kukataa wito wangu, basi hayo hayatanidhuru mimi kitu. Kwani mimi sikufanya hivyo kwa kutaraji kupokea ujira kwenu ambao naogopa nitaukosa, kwa sababu ya kukataa kwenu! Ujira wangu mimi nautaka kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na Yeye ameniamrisha niwe Muislamu, nimsalimishie Yeye mambo yangu yote.
Na juu ya juhudi hizo, na kukakamia huko aliko kakamia Nuhu kwa ajili ya kutaka kuwaongoa hao watu wake, bado walishikilia kuendelea na kumkanusha na kumfanyia uadui. Basi Mwenyezi Mungu alimwokoa yeye pamoja na wenye kumuamini, wakapanda marikebu. Na akawajaalia hao ndio walio iamirisha nchi baada ya kuteketea makafiri, walio gharikishwa na tofani. Hebu angalia, ewe Muhammad! Vipi walio puuza onyo ulivyo malizikia mwisho wao mbaya.
Baada ya Nuhu tuliwatuma Mitume wengine wakilingania Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu, wakibashiria kheri na wakionya, na wakiungwa mkono na miujiza yenye kuonyesha ukweli wao. Watu wao wakawakanya kama walivyo kanya kaumu ya Nuhu. Haukuwa mwendo wa wapinzani kuwa wat'iifu, kwa sababu kule kukadhbisha kwao kulikuwa ni mbele kuliko kuzingatia na kupima. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu alipiga muhuri wa upotovu juu ya nyoyo za wale ambao mtindo wao ni kuzifanyia uadui hakika na Ishara zilizo wazi!
Kisha baada yao tulimtuma Musa na ndugu yake Haruni wende kwa Firauni, mfalme wa Misri na watu wake wakuu makhsusi, kuwaita wamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake. Nao waliungwa mkono na hoja zenye nguvu. Firauni na kaumu yake walitakabari wakakataa kuitikia wito wa Musa na Haruni. Kwa kukataa kwao huko wakawa wamefanya makosa makubwa na dhambi.
Ilipo dhihiri Haki yetu kwa mkono wa Musa, ule muujiza wa Musa - nao ni fimbo kugeuka nyoka mbele ya macho yao - wao walisema: Hakika huu ni uchawi ulio dhaahiri!
Musa akawaambia kukanya uzushi wao: Nyinyi mnaita Haki iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni uchawi? Hivyo hii kweli mliyo iona kwa macho yenu ni uchawi? Basi hivi hapa mimi nakutakeni mthibitishe kwamba huu ni uchawi. Waleteni wachawi wathibitishe hayo mnayo yadai. Na wachawi hawafanikiwi abadan!
Firauni na watu wake walimwambia Musa: Hapana shaka wewe umekuja kwa makusudi ya kutuachisha dini ya baba zetu, na mila za kaumu yetu, ili nyinyi wawili mpate kuwa na wafuasi; wewe na nduguyo mpate ufalme na utukufu na urais wa kutawala na kuhukumu! Kwa hivyo basi sisi hatutakuaminini nyinyi wala huo utume wenu!