Hakika wale wasio amini kufufuliwa na kukutana na Mwenyezi Mungu Siku ya Mwisho, na wakaamini - kwa kudhani tu - kuwa uhai wa duniani ndio mwisho wao na hapana baada yake uhai mwingine, na wakatulia nyoyo zao kwa hayo, na wala wasijue nini kitakuwa baada yake, na wakaghafilika na Ishara za Mwenyezi Mungu juu ya kufufuliwa na kuhisabiwa,
Hakika walio amini Imani ya kweli kweli, na wakatenda mema katika dunia yao, Mola wao Mlezi atawathibitisha kwenye Uwongofu kwa sababu ya Imani yao, na Siku ya Kiyama atawatia katika Bustani zipitazo mito kati yake, na wataneemeka kwa neema za milele.
Dua za Waumini katika Bustani hizo ni kumsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila waliyo kuwa wakiyasema makafiri duniani, na kusalimiwa na Mwenyezi Mungu, na kusalimiana wao kwa wao ili kuthibitisha amani na utulivu. Na kukhitimishia dua yao ni kumhimidi Mwenyezi Mungu kwa tawfiqi yake, kuwawezesha, kufikia Imani na kufuzu kwao kuipata radhi yake.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli waitikia watu wanapo jiapizia shari kama vile wanavyo jihimizia kuitaka kheri, angeli waangamiza akawateketeza wote. Lakini Yeye anawachukulia kwa upole basi anaakhirisha kuwateketeza, ili kungojea wadhihirishe walio nayo kwa mujibu wa anavyo wajuulia, upate kuonekana wazi uadilifu wake kwa atavyo walipa. Wanaachwa na ushahidi wa kutosha umesimama dhidi yao, nao makusudi wanakengeuka na kuelekea njia ya upotovu na udhalimu.
Na mtu akisibiwa na madhara katika nafsi yake au mali yake au mfano wa hayo, huhisi unyonge wake, na humwomba Mola wake Mlezi kwa hali yoyote - akiwa kajinyoosha, au kakaa kitako, au kasimama - amwondolee dhiki zake! Mwenyezi Mungu akisha mwitikia, na akamwondolea hizo shida zake, humuacha kando Mwenyezi Mungu na akaendelea na maasi yake, na akasahau fadhila za Mwenyezi Mungu juu yake, kama kwamba hakupatikana na madhara yoyote, wala hajapata kumwomba amwondolee! Na mfano wa mtindo huu Shetani ndio huwazaini Makafiri, akawapambia vitendo vyao viovu, na uzushi wao mpotovu, wakaona yote hayo ni mazuri.
Na Sisi tulikwisha ziangamiza kaumu zilizo kutangulieni kwa sababu ya kufuru zao walipo wajia Mitume na Ishara zilizo wazi za kusadikisha wito wao wa kuitia Imani. Na Mwenyezi Mungu akijua, kwa ajili ya kung'ang'ania kwao ukafiri na uasi, kuwa haitopatikana Imani kwao! Basi enyi makafiri wa Kikureshi! Zingatieni! Kama tulivyo waangamiza walio kuwa kabla yenu, kadhaalika tutawalipa wakosefu kwa maangamizo.
Enyi Umma wa Muhammad! Tumekujaalieni muwe makhalifa wa ardhi, mshike pahala pa walio kutangulieni, ili tukujaribuni tudhihirishe mtacho kikhiari, ut'iifu au uasi, baada ya mlivyo kwisha jua yaliyo wapata walio kutangulieni.