Walipo kwenda naye mbali na baba yake, na wakakubaliana rai yao ya kumtumbukiza ndani ya kisima, walifanya hayo waliyo yaazimia. Sisi tukamtia moyoni mwake Yusuf atulie, na awe na imani ya Mwenyezi Mungu, kuwa bila ya shaka atakuja waeleza haya mambo yao waliyo yapanga na wakayatenda, na wala wao wenyewe hawajui hapo utapo waambia kwamba wewe ndiye Yusuf waliye mfanyia vitimbi, na wakadhani wamekwisha mmaliza na wameepukana naye!
Wakasema: Ewe baba yetu! Sisi tulikwenda kushindana kupiga mishale na kwenda mbio, na tukamwacha Yusuf kwenye vitu vyetu avilinde. Mbwa mwitu akamla, na sisi tuko mbali tumeshughulika na mashindano! Na wewe hutusadiki tunayo yasema, ijapokuwa tunasema haki na kweli!
Wakaileta kanzu yake nayo ina damu, ati kuwa ni ushahidi wa yale madai yao ya kuwa ile ni damu ya Yusuf, apate kusadiki baba yao! Walakini yeye alisema: Hakika huyo mbwa mwitu hakumla kama mnavyo singizia, bali nafsi zenu zimekupelekeeni kufanya jambo kubwa, na mkalitimiza! Langu mimi ni kusubiri subira njema isiyo legalega kwa mliyo nikutisha. Na Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye takiwa msaada kwa huo upotovu mlio uzua na mnao udai.
Wakaja watu upande ule wa kisima katika msafara wao wa kwendea Misri. Wakamtuma mtu kati yao wa kuchota maji kisimani awaletee. Akatumbukiza ndoo yake, akiivuta na Yusuf kang'ang'anilia! Yule mchota maji akapiga kelele za furaha: Kheri! Kheri gani hii na furaha! Huyu ni kijana! Wakamficha katika vitu vyao, wakamfanya ni bidhaa ya biashara! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyazunguka yote wayatendayo kwa ujuzi wake.
Wakamuuza Misri kwa bei ya chini kabisa, si kiasi chake! Thamani yake ilikuwa ni pesa chache tu! Wala hawakuwa wakimtakia Yusuf thamani kubwa, kwa kukhofia wasije watu wake wakamkuta wakamtambua, na wakawapokonya Yusuf.
Yule aliye mnunua kule Misri alimwambia mkewe: Mfanyie wema huyu, na umhishimu, ili makao yake hapa nasi yawe mazuri. Huenda akatufaa, au tukamfanya kuwa ni mwenetu. Kama yalivyo kuwa makaazi yake ni mazuri na ya hishima, basi kadhaalika tulimjaalia Yusuf katika nchi ya Misri cheo kingine kikubwa, ili atekeleze uadilifu na mipango mizuri, na ili tumfunze kufasiri mambo na ndoto, ajue yatakayo kuwa kabla hayajwa, ili awe tayari kuyakabili! Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kutimiza kila jambo alitakalo. Kabisa haemewi na kitu. Lakini watu wengi hawajui siri ya hikima yake, na undani wa mipango yake.
Na Yusuf alipo timia ukomo wa nguvu zake tukampa hukumu yenye kusibu, na ilimu yenye kufaa. Na kama malipo haya tuliyo mpa yeye kwa wema wake, ndio tunavyo wapa wote walio wema kwa vitendo vyao vyema.