Baba yake akamwambia: Ewe mwanangu! Usiwasimulie nduguzo ndoto yako hii. Itakuja watia husda katika nyoyo zao, na Shetani atawachochea wazue njama kukupinga. Watakuja kufanyia hila na vitimbi! Hakika Shetani ni adui wazi wa binaadamu!
Kama ulivyo jiona katika ndoto kuwa ni bwana wa kut'iiwa, mwenye cheo na madaraka, basi Mola wako Mlezi atakuteuwa na atakukhitari, akufunze kufasiri ndoto, kwa kukupa Unabii na Utume, kama hapo zamani, kabla ya baba yako, Yaa'qub, alivyo wafanyia baba zako, Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni mwingi wa hikima, basi hakosei. Ni mwingi wa ujuzi, basi humteuwa katika waja wake anaye mjua kuwa anastahili kuteuliwa.
Walipo semezana nduguze Yusuf kwa baba: Bila ya shaka Yusuf na nduguye kwa baba na mama wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi. Na sisi ni kikundi chenye nguvu, chenye kumfaa yeye zaidi kuliko wao! Hakika baba yetu kwa kumfadhilisha Yusuf na nduguye kuliko sisi yumo makosani, na yuko mbali na haki. Yalio sawa yapo wazi yanaonekana.
Muuweni Yusuf, au mtupeni nchi iliyo mbali na baba yenu, asiyo weza kuifikia. Yatakuwafikieni nyinyi tu mapenzi ya baba yenu, na atakuelekeeni nyinyi tu. Na baada ya kumtenga Yusuf naye kwa kumuuwa au kumhamisha mtakuwa watu wema. Kwani Mwenyezi Mungu atakubali toba yenu, na baba yenu atapokea udhuru wenu.
Mmoja wao katika wasemaji alisema: Msimuuwe Yusuf. Hayo ni makosa makubwa. Lakini mtupeni asipo onekana ndani ya kisima, baadhi ya wapita njia watakuja mwokota, watapo tumbukiza ndoo yao kisimani. Hao watakwenda naye pahala pambali nanyi na baba yenu vile vile. Haya ikiwa nyinyi mna lazima mumpeleke mbali na mtimize kwa kitendo hayo mtakayo.
Baada ya kuwafikiana kumbaidisha Yusuf (kumpeleka mbali) walisema: Ewe baba yetu! Nini kinacho kutia shaka nasi hata unamtenga Yusuf nasi, wala huoni pana usalama anapo kuwa nasi? Sisi tunakuhakikishia kuwa sisi tunampenda, na tunamwonea huruma, na tunamtakia kheri, na tunamwongoza kwenye kheri. Hapati kwetu isipo kuwa mahaba, na nasiha safi kabisa.
Mwache ende nasi kesho machungani. Atastarehe kwa kula vyakula vizuri, atacheza na atafurahi. Na sisi kwa yakini tuna hima ya kumhifadhi kumkinga na madhara yoyote.
Mzee akasema: Hakika mimi naona huzuni mkiondoka naye, akawa mbali nami. Na nina khofu nikikuaminini asije akaliwa na mbwa mwitu na nyinyi mmeghafilika naye.
Wakasema: Tunakuapia, akiliwa na mbwa, na hali sisi ni kundi lenye nguvu, basi itakuwa ni fedheha na khasara kwetu! Likitokea hilo unalo liogopa basi sisi tutakuwa tumekhasiri kila linalo pasa kulishughulikia, na kuwa lisitokee. Basi tuwa kwa hayo! Hatutadharau kumlinda, ikiwa hivyo itakuwa tunajipelekea wenyewe kupotea na kupuuza.