Waombee msamaha hao wanafiki, ewe Mtume, au usiwaombee msamaha, Mwenyezi Mungu Hatawasamehe, namna yatakayokuwa mengi na kukaririka maombi yako kutaka wasamehewe, kwa kuwa wao wamemkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Hawaafikii kwenye uongofu wale waliotoka nje ya utiifu Wake.
Walifurahi wale waliojiweka nyuma wasimwandame Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani ziwashukiye, kwa kujikalia Madina wakienda kinyume na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na walichukia kupigana jihadi pamoja na Yeye kwa mali zao na nafsi Zao katika njia ya Mwenyezi Mungu na waliambiana wao kwa wao, «Msitoke katika kipindi cha joto.» Waambie, ewe Mtume, «Moto wa Jahanamu una joto zaidi,» lau wao wanalijua hilo.
Basi na wacheke hao wanafiki waliojiweka nyuma wasimwandame Mtume wa Mwenyezi Mungu katika vita vya Tabūk, kidogo katika uhai wao wa kilimwengu wenye kumalizika, na walie sana katika Moto wa Jahanamu, ukiwa ni malipo ya yale ambayo walikuwa wakiyachuma duniani ya unafiki na ukafiri.
Basi Akikurudisha Mwenyezi Mungu, ewe Mtume, kutoka kwenye vita ulivyopigana ukaja kwenye kundi la wanafiki waliothibiti juu ya unafiki, na wakakutaka ruhusa watoke na wewe kwenye vita vingine baada ya vita vya Tabūk, waambie, «Hamtatoka pamoja na mimi kabisa kwenye vita vyovyote, na hamtapigana pamoja na mimi na adui yoyote. Nyinyi mumeridhika kukaa mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na wale waliojiweka nyuma wakaacha kupigana jihadi pamoja na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.»
Na usimswalie kabisa, ewe Mtume, yoyote aliyekufa miongoni mwa wanafiki na usisimame kwenye kaburi yake kumuombea, kwa kuwa wao wamemkanusha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wamekufa na wao wametoka kwenye utiifu. Hii ni hukumu yenye kuenea kwa kila mtu ambaye unafiki wake umejulikana.
Na zisikushangaze mali za wanafiki hawa na watoto wao. Mwenyezi Mungu Anataka kuwaadhibu wao kwa hizo ulimwenguni, kwa kupambana kwao na shida katika kuzipata na kwa kufa kwao katika hali ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Na pindi sura yoyote ikiteremshwa kwa Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, inayoamrisha kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtakasa na kupigana jihadi pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, wale wenya uwezo wa kifedha miongoni mwa wanafiki wanakuomba ruhusa na wanasema, «Tuache pamoja na waliokaa wasioweza kutoka.»