Hili ni elezo la kujiepusha litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na ni tangazo la kuachana kabisa na makubaliano yaliyokuwako kati ya Waislamu na Washirikina.
Tembeeni, enyi washirikina, katika ardhi muda wa miezi minne, mutembee mnapotaka mkiwa kwenye amani bila kusumbuliwa na Waumini, na mjue kwamba nyinyi hamtayaponyoka mateso. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwatweza Makafiri na ni Mwenye kuwatia aibu hapa ulimwenguni na Moto kesho Akhera. Aya hii inawahusu wale waliokuwa na mapatano huru yasiyokuwa na muda au yule ambaye alikuwa kwenye makubaliano chini ya miezi mine, akamilishiwe miezi yake minne, au aliyekuwa na mapatano akayavunja.
Na ni ujulisho kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni onyo kwa watu siku ya kuchinja kwamba Mwenyezi Mungu Amejitenga na washirikina; na Mtume Wake pia Amejitenga na wao. Basi ikiwa mtarudi kwenye haki, enyi washirikina, na mkauacha ushirikina wenu, hilo ni bora kwenu. Na mkiipa mgongo haki kwa kutoukubali na mkakataa kuingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu, basi jueni kwamba nyinyi hamtaiponyoka adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na waonye, ewe Mtume, hawa wenye kuupa mgongo Uislamu, adhabu ya Mwenyezi Mungu iumizayo.
Na wanavuliwa, kwenye hukumu iliyopita, washirikina walioingia pamoja na nyinyi kwenye makubaliano yenye muda ujulikanao, na wakawa hawakufanya hiana kwenye mapatano, wala hawakumsaidia yoyote katika maadui, basi watimizie ahadi yao mpaka mwisho wake uliowekwa Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wachamungu ambao wanatekeleza waliyoamrishwa. Na ogopeni ushirikina na uhaini na maasia mengineyo.
Basi pindi itakapomalizika miezi minne, ambayo ndani yake mliwapa amani washirikina, basi tangazeni vita juu ya maadui wa Mwenyezi Mungu popote walipo, na muwalenge kwa kuwazingira kwenye vituo vyao na muwavizie kwenye njia zao. Na iwapo watarudi nyuma kuacha ukafiri wao, wakaingia kwenye Uislamu na wakajilazimisha na sheria zake za kusimamisha Swala na kutoa Zaka, basi waacheni, kwani wameshakuwa ndugu zenu katika Uislamu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waliotubia na wakarudi nyuma, ni Mwenye huruma kwao.
Na pindi yoyote, miongoni mwa washirikina ambao damu zao na mali zao zimehalalishwa, akiomba kuingia kwenye himaya yako, ewe Mtume, na akataka amani, basi mkubalie maombi yake ili apate kuisikia Qur’ani tukufu na auone uongofu wake, kisha mrudishe alikotoka akiwa kwenye usalama. Hilo ni kwa sababu ya kumsimamishia hoja, kwa kuwa Makafiri hawaujui uhakika wa Uislamu, kwani huenda wakauchagua pindi ujinga wao ukiwaondokea.