Si haki kwa yoyote aliyeamini kumfanyia uadui ndugu yake aliyeamini kwa kumuua bila haki isipokuwa afanye hilo kimakosa kwa kutokusudia. Na yoyote ambaye kosa hilo lilitokea kwake, basi ni juu yake aache huru shingo iliyoamini na atoe dia iliyokadiriwa kiwango chake kuwapa mawalii wa aliyeuawa, isipokuwa iwapo watamuachia kwa njia ya sadaka na watamsamehe. Iwapo muuliwa anamuamini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na anaiamini haki aliyoteremshiwa Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na akawa ni katika ukoo wa watu makafiri ambao ni maadui wa Waislamu, basi ni juu ya muuaji aache huru shingo iliyoamini. Na iwapo muuliwa ni miongoni mwa watu ambao baina yenu na wao kuna ahadi na mapatano, basi ni juu ya yule aliyemuua, ili Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amkubalie toba yake, aache huru shingo iliyoamini; asipopata uwezo wa kuacha huru shingo iliyoamini, ni juu yake afunge miezi miwili yenye kufuatana. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ni Mjuzi wa hakika ya mambo ya waja Wake, ni Mwenye hekima katika sheria Zake Alizowawekea.
Na mwenye kumfanyia uadui Muumini akamuua kwa kusudi pasi na haki, mwisho wake atakaoishia ni Jahanamu, hali ya kukaa milele humo, pamoja na kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kufukuzwa kwenye rehema Yake, iwapo Mwenyezi Mungu Atamlipa kwa kosa lake. Na Mwenyezi Mungu Amemuandalia adhabu kali zaidi kwa uhalifu huu mkubwa aliyoufanya. Lakini Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Atawasamehe na kuwafadhili wenye Imani kwa kutowapa malipo ya kukaa milele ndani ya Jahanamu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, mnapotoka kwenye ardhi hali ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuweni na uangalifu wa mnayoyafanya na mnayoyaacha. Na msimkanushie Imani yoyote ambaye imedhihiri kwake chochote katika alama za Uislamu na akawa hakuwapiga vita nyinyi, sababu pana uwezekano ya kuwa yeye ni Muumini anayeificha Imani yake. Msifanye hivyo kwa kutaka starehe za uhai wa kilimwengu kwani kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka pana nyongeza na vipewa vinavyowatosha. Na nyinyi mlikuwa hivyo mwanzo wa Uislamu, mkiificha Imani yenu kwa jamaa zenu washirikina, kisha Mwenyezi Mungu Akawaneemesha na Akawatukuza kwa Imani na kwa nguvu Alizowapa. Basi kuweni kwenye ubainifu na ujuzi katika mambo yenu. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa matendo yenu yote, ni Mwenye kuyaona mambo yenu ya ndani, na Atawalipa kwayo.