Na Kumbukeni neema yetu kwenu, tuliposema, “Ingieni mji wa Baitul Maqdis na kuleni vizuri vyake, mahali popote pa mji huo, kwa starehe. Na muwe, katika kuingia kwenu, wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, wadhalilifu Kwake na mseme, ‘Ewe Mola wetu, tuondolee madhambi yetu,’ tutawaitikia, tutawasamehe na kuyafanya yasitirike.” Na wenye Kufanya wema katika amali zao tutawazidishia kheri na thawabu.
Wale wajeuri waliyo wapotevu, katika wana wa Isrāīl, walibadilisha neno la Mwenyezi Mungu na wakaipotoa kauli pamoja na kitendo. Kwani waliingia, na huku wakijikokota kwa matako na wakisema, “habbah fī sha’rah’ (mbegu unyweleni.)”, wakiifanyia maskhara dini ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Aliwateremshia adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya kuasi kwao na kutoka kwao kwenye utiifu kwa Mwenyezi Mungu.
Na Kumbukeni neema Yetu kwenu, mlipokuwa na kiu katika kuzunguka kwenu, alipotuomba Musa, kwa unyenyekevu, tuwaletee maji watu wake. Tukasema, “Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako.” Akalipiga, na chemchemi zikabubujika hapo jiweni sehemu kumi na mbili, ikilingana na idadi ya makabila yao, pamoja na kulijulisha kila kabila chemchemi yake ya kutumia, ili wasigombane. Na tukawaambia, “Kuleni na kunyweni riziki ya Mwenyezi Mungu wala msitembee katika ardhi kuleta uharibifu.”
Na Kumbukeni, tulipowateremshia chakula tamu na ndege wa kuvutia, mkawa hamjali, kama ilivyo desturi yenu, ikawapata dhiki na machovu na mkasema, “Ewe Mūsā! Sisi hatutavumilia chakula hicho kwa hicho kisichobadilika siku zote. Basi tuombee Mola wako Atutolee chakula katika mimea ya ardhini kama mboga, matango, mbegu zinazoliwa, adasi na vitunguu.” Musa akawaambia, kwa kuwapinga vikali, “Vipi mnataka hivyi ambavyo ni duni zaidi na mnaacha riziki yenye manufaa ambayo Mwenyezi Mungu amewachagulia? Ondokeni jangwani na mshuke mjini. Huko mtavipata mnavyovitamani sana kwenye mashamba na masoko.” Waliposhuka, iliwabainikia kuwa wao wanatanguliza chaguo lao,kila mahali, juu ya chaguo la Mwenyezi Mungu na wanayafadhilisha matamanio yao juu ya vitu ambavyo Mwenyezi Mungu Alilowachagulia. Kwa hivyo, sifa ya unyonge na umasikini wa moyo iliwaambata, na wakaondoka na kurudi wakiwa wamo kwenye ghadhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuipa mgongo dini ya Mwenyezi Mungu, na kwa kuwa wao walikuwa wakikanusha aya za Mwenyezi Mungu na kuua Manabii kwa udhalimu na uadui. Yote hayo ni kwa sababu ya kuasi kwao na kuivuka mipaka ya Mola wao.