Ewe Nabii! Sisi hatukumtuma Mtume yeyote kabla yako ila tulimpa wahyi (ufunuo) awafikishie watu wake kuwa hastahiki kuabudiwa isipo kuwa Mimi. Basi nisafieni ibada, iwe kwangu tu.
Na baadhi ya makafiri wa Kiarabu walisema: Arrahman, Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, ana mwana, kwa yale madai yao kuwa Malaika ni binti za Mwenyezi Mungu. Ametakasika na kuwa na mwana! Kwani hao Malaika ni waja wake walio tukuzwa tu kwa kuwakaribisha, na kwa wanavyo muabudu Yeye.
Hawamtangulii Mwenyezi Mungu kwa kauli yao wainenayo kabla ya Yeye kuwapa ruhusa. Na wao hawatendi lolote ila kwa amri yake tu, wala hawapindukii mipaka ya amri anayo waamrisha.
Mwenyezi Mungu anazijua hali zao zote na vitendo vyao vyote, walivyo vitanguliza na walivyo viakhirisha. Wala hawamwombei mtu kwake ila kwa aliye ridhia Mwenyezi Mungu. Na wao jinsi ya wingi wa khofu yao kumwogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kumtukuza Yeye, daima wana hadhari naye..
Na miongoni mwa Malaika atakaye sema: Mimi ni mungu wa kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, huyo tutamlipa kwa kumtia Jahannamu. Mfano wa malipo hayo tunamlipa kila mwenye kupindukia mipaka ya haki, na wakajidhulumu nafsi zao kwa kudai Ungu na kuingia katika ushirikina.
Wenye kukufuru wamepofuka, na hawaoni kuwa mbingu na ardhi hapo mwanzo zilikuwa zimeshikamana. Kwa uwezo wetu tukazibambandua mbali mbali. Na tukajaalia kutokana na maji, ambayo hayo si kitu hai, kila chenye uhai kutokana na hayo hayo. Basi je! Baada ya yote haya wangali kupuuza tu, na hawaamini kuwa bila ya shaka yoyote hapana mungu isipo kuwa Sisi? "Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini?" Aya hii ina maana ya kisayansi yenye kutilia nguvu nadhariya ya ilimu za kisasa katika kuumbwa sayari na ardhi. Nayo ni kuwa mbingu na ardhi asili yao zilikuwa zimeshikamana. Na ukweli wa sayansi zinazo kubaliwa ni kuwa hakika ziliambatana, na sayansi mbali mbali zinathibitisha hayo. Na zipo nadhariya nyengine kadhaa wa kadhaa ambazo kwazo zaweza kuelezea dhaahiri ya mambo haya. Lakini bado kuthibiti nadhariya mojapo kwa njia ya mkato kwa wanazuoni kwa kuwafikiana wote. Kwa kuonyesha mfano tutaja nadhariya mbili: Nadhariya ya Kwanza: Imekhusu kuumbwa kwa mfumo wa jua (Solar System). Kwa mfano imethibiti kuwa mawingu au umande ulio zunguka jua ulianza kuenea kwenye anga lilio baridi, na chembechembe za gasi zinazo fanya hayo mawingu au moshi zikakusanyika kwenye chembechembe za vumbi linalo kwenda kwa kasi kubwa. Kisha chembechembe hizo zikawa zinagongana na zinarindika, na huku ndani yake zikawamo gasi nzito, na kukazidi kurindika na kujumuika kwa kupita mamilioni na mamilioni ya makarne mpaka zikafanyika sayari na mwezi na ardhi kwa umbali unao stahiki. Na yajuulikana kuwa huko kukusanyika na kurindika huzidisha mbinyo (Pressure), na huo huzidisha joto. Na gamba la ardhi lilipo ingia kupoa, na wakati zilipo ripuka volkano ardhi ikapata mvuke wa maji na gasi ya Carbon dioxide ilio tokana na miripuko ya volkano...na katika iliyo saidia kupatikana Oxygen katika hewa baada ya hapo ni nishati na nguvu za miyale ya jua kwa njia ya mwanga juu ya mimea na majani ya mwanzo. Ama Nadhariya ya Pili: Imekhusiana na uumbaji wa ulimwengu kwa jumla, ambao kwa mukhtasari unaelezwa na kauli yake Mtukufu: "Zilikuwa zimeambatana", yaani zimeshikamana na kuwa kitu kimoja. Na hayo ndiyo yaliyo fikilia mwishoni ilimu za sayansi katika uumbaji wa ulimwengu. Nayo ni kwamba kabla ya kufikilia sura yake hii ya sasa ulikuwa kama donge lilio kusanyika lenye kutisha, la mkusanyiko wa chembechembe zenye kuambatana chini ya mbinyo pressure, hata akili haiwezi kuifikiria. Na hizi sayari zote na nyota zilioko mbinguni hivi leo tunazo ziita mfumo wa jua solar system zilikuwa ni mkusanyiko wa donge moja lisilo zidi 1/2 diameter yake maili milioni tatu. Na neno lake Mwenyezi Mungu: "Tukazibambandua" linafahamisha ule mripuko mkubwa wa mwanzo wa ki-nuclear ukazalisha uumbaji wa anga na sayari za namna mbali mbali tunazo ziita kwa pamoja "Mfumo wa Jua" au Solar System. "Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai": Aya hii imethibitisha uhakika wa kisayansi ulio thibitishwa na ncha mbali mbali za ilimu. Imethibitisha Cytology, sayansi ya "cells", (khalaya), kwamba maji ni muhimu kabisa katika ujengaji wa "cells" zote za vitu vilivyo hai, ikiwa mimea au wanyama. Na ilimu ya "Kimyaa", Chemistry kwamba maji ni lazima yapatikane katika vitendo na mageuko yoyote katika viumbe vilivyo hai. Basi hayo maji ama yawe ni kiungo, kitu cha kusaidia, au cha kuwamo ndani ya kitendo, au ni matokeo yake. Na imethibitisha ilimu ya viungo physiology kwamba maji ni dharura kwa viungo kufanya kazi yao. Bila ya hayo maji hautodhihiri uhai katika viungo.
Na katika dalili za uweza wetu ni kuwa tumeifanya milima imesimama imara kwenye ardhi ili isiyumbeyumbe nao watu, na tumefanya humo njia pana, za kupitia kwa wasaa, ili waweze kuongoza njia humo kwa makusudio yao. Maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 31: "Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka." Ilivyo kuwa ndani ya ardhi kila kitu kimeyayuka, na lau kuwa milima imewekwa tu katika baadhi ya sehemu za huu mpira wa dunia kama majabali yaliyo nyanyuka juu tu, uzito wao ungeli sabibisha gamba la dunia liyumbe, au lipindane na kupasuka. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu kwa utukufu wa shani yake ameifanya milima isimame imara kwa kuwa na mizizi iliyo zama kwenye gamba la ardhi mpaka chini kwenye kina kirefu kulingana na urefu wake kwendea juu. Kwa hivyo imekuwa hiyo milima kama vigingi, kama alivyo jaalia eneo la minyanyuka hii na mizizi ni duni kuliko maeneo ya gamba lilio zunguka. Yote haya ni kwa ajili ya kueneza sawa uzito wa juu ya gamba kwa pande zote ili pasiwepo kuyumbayumba na kupasuka. Kwani hakika kuenezwa kwa uzito juu ya uso wa dunia yakaribia kuwa hakuleti athari kubwa ya kutajika. Na ilimu za kisasa zimethibitisha kuwa kuenezwa kwa nchi kavu na maji juu ya ardhi, na kuwepo mfululizo wa milima juu yake ni katika yanayo hakikisha hali ilivyo ardhi, na imethibitika kuwa chini ya milima mizito kuna vitu vyepesi kubungunyika, na chini ya maji ya bahari kuu vipo vitu vizito. Kwa kuenezwa uzani wa namna hiyo mbali mbali katika dunia, na mgawanyo huu wa milima, makusudio yake ni kusawizisha uzani wa mpira huu wa ardhi. Na ilivyo nyanyuka milima zikatokea nyanda na mabonde na njia baina ya milima na mwambao na bahari na minyanyuko, na zikawa njia.
Na tumeifanya mbingu kama dari iliyo nyanyuliwa, na tukailinda isianguke, au visianguke viliomo humo. Na juu ya hayo, wao hawazioni wala hawaziingatii Ishara zetu zenye kuonyesha uweza wetu na hikima yetu na rehema yetu. Maoni ya wataalamu juu ya Aya 32: "Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa lakini wanazipuuza Ishara zake. ": Aya hii tukufu imethibitisha kuwa mbingu na vyote viliomo ndani yake vimehifadhiwa visiwe na ila yoyote, na vimehifadhiwa visidondoke juu ya ardhi. Na mbingu ni kila kilicho juu yetu, kuanzia kifuniko hichi cha hewa inayo walinda walioko juu ya ardhi na khatari nyingi za angani ambazo zinazuia maisha, mfano wa vimondo vya nyota za mkia, na miyale. Na juu ya ardhi pana kifuniko cha hewa kinacho linda ardhi kwa nguvu za mvutano, na haifai kukosekana hivyo bila ya maangamizo kabisa. Na juu ya kifuniko cha hewa ndio kuna hizo sayari za mbinguni, na zipo kwa umbali mbali mbali kufuatana na nyendo zao tangu mwanzo. "Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa" yaani hizo sayari na vyote vilio mbinguni vyaonekana kwa nadhari yetu kama kwamba ni dari, na tunaona vilio juu ya vichwa vyetu kama ni vidogo kuliko vilioko upeo wa macho. Na hayo ni kiini macho tu, kama tunapo liona jua kubwa wakati wa kuchomoza na kuchwa kuliko adhuhuri. Na hili qubba la mbingu lina sifa zake, zinazo khitalifiana kila ukizidi mnyanyuko wa ardhi, kama hizo sayari za mbinguni kwa mujibu wa jicho linavyo ona katika qubba la mbingu.
Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba usiku na mchana, na jua na mwezi. Vyote hivyo vinakwenda katika njia zake kama alivyo zijaalia Mwenyezi Mungu, na zinamtakasa bila ya kupotea. Maoni ya wataalamu juu ya Aya 33: "Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea." Kila sayari ya mbinguni ina mzunguko wake makhsusi inayo ogelea kuufuata. Na zote hizo hazisiti, na zinakwenda kwa mwendo wao maalumu katika anga. Na sisi tunaona hayo kwa hakika kwa kutazama mwendo wa jua na mwezi. Kama kadhaalika mzunguko wa ardhi wake wenyewe ndio unao leta usiku na mchana kwa zamu, kama kwamba unaogelea.
Ewe Nabii! Hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako wewe aishi milele, hata ikawa hao makafiri wakawa wanakutamania ufe wewe. Vipi wanakutamania mauti wewe na hali na wao vile vile watakufa kama wewe? Ukifa wewe, je, ndio wao watabakia kushinda wanaadamu wote?
Kila nafsi haina budi kuonja mauti. Na Sisi tunakufanyieni hapa duniani kama wenye kukupeni mtihani, kwa kukupeni yenye manufaa yenu na yenye madhara pia, ili abagulike mwenye kushukuru kwa kupewa kheri na kuvumilia balaa, na yule asiye na fadhila kwa neema aipatayo na anapapatika akipata misiba. Nanyi mtarejeshwa kwetu, na hapo tutakuhisabieni vitendo vyenu.