Enyi mlio amini! Piganeni na makafiri walio karibu yenu ili wasiwe ndio sababu ya kukutieni khatarini. Na kueni wakali kwao mnapo pigana, wala msiwafanyie upole. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu kwa msaada wake na nusra yake yu pamoja na wanao mcha.
Na ikiteremka Sura ya Qur'ani wakaisikia wanaafiki huifanyia maskhara na kuikejeli. Huambizana wao kwa wao: Nani katika nyinyi iliyo mzidisha Imani? Ndio Mwenyezi Mungu anawajibu ya kwamba ipo farka baina ya wanaafiki na Waumini. Ama Waumini ndio wale walio iona Nuru na wakaijua Haki. Hao Aya za Mwenyezi Mungu zimewazidishia Imani, na wao huzifurahia wakati zinapo teremka.
Ama wanaafiki ambao nyoyo zao zinaugua, na macho yao yamepofoka, hao haziwazidishi ila ukafiri juu ya ukafiri walio nao, na watakufa hali nao ni makafiri.
Je! Hawazingatii wanaafiki vile Mwenyezi Mungu anavyo wapa majaribio kila mwaka mara moja au zaidi, kwa balaa namna mbali mbali, kama kuwakashifu siri zao, na kudhihirisha hali zao na kushindwa na Waumini, na kufichuliwa upotovu wao? Kisha juu ya yote hawaachi hao walio nayo wakatubu, wala hawayakumbuki yanao wapata.
Na kadhaalika ikiteremka Sura nao wapo barazani kwa Mtume hukonyezana na kuambiana: Yuko mtu anaye kuoneni? Tena nyoyo zao hukengeuka wasimfuate Mtume wala wasimuamini! Mwenyezi Mungu amewazidisha kupotea kwa vile kushikilia kwao kubaki katika upotovu na kuikataa Haki, kwani watu hawa hawafahamu kitu!
Enyi watu! Amekujieni Mtume, binaadamu kama nyinyi kwa umbo lake. Anapata dhiki kwa madhara yanayo kusibuni, ana hamu mwongoke, na mwingi wa huruma na rehema kwa Waumini.
Basi, ewe Mtume! Wakiipuuza Imani, wakaikataa, wewe usihuzunike kwa mapuuza yao. Wewe tafakhari na utukufu wa Mola wako Mlezi, na useme: Ananitosheleza Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu asiye kuwa Yeye. Juu yake Yeye tu peke yake mimi nategemea. Na Yeye ndiye Mmiliki wa ufalme wote, Mola Mlezi wa viumbe vyote, na ndiye Mwenye utawala mkuu.