Haitofaa kitu kuwaitikia baadhi yao na ukawaombea maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Ewe Nabii! Ukiwaombea msamaha au ukitowaombea, hata ukiwaombea mara ngapi, Mwenyezi Mungu hatowasamehe! Kwa sababu kwa hawa hapana matarajio ya msamaha wala maghfira maadamu wanaendelea na ukafiri wao. Na watu hawa wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wanao kwenda kinyume naye, wakamuasi, na wakenda kinyume na kumuasi Mtume wake, na wakaiasi Sharia yake na Dini yake.
Hakika wanaafiki walibaki nyuma wasitoke pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenda kuwakaabili maadui, na wakafurahi kubakia Madina baada ya kutoka Nabii, na kukhalifu amri yake ya kwenda kwenye Jihadi. Walichukia kutumia mali yao na kujitolea roho zao kwa ajili ya Jihadi kulinyanyua Neno la Mwenyezi Mungu na kuinusuru Dini yake. Wakawa wao wakiwavunja moyo wengineo, na wakiwashawishi wabaki nyuma pamoja nao, na wakiwatisha wasende vitani katika joto kama hilo! Ewe Mtume! Waambie hawa: Kama nyinyi mna akili mtakumbuka kuwa vukuto la Moto wa Jahannamu ni kali zaidi na lina shida zaidi kuliko hili mnalo likhofu.
Basi nawacheke kufurahia kutokwenda vitani na kuwakejeli Waumini. Kwani kicheko chao muda wake ni mfupi; kitakwisha yatakapo kwisha maisha yao hapa duniani. Tena kitafuata kilio kikubwa kisicho kuwa na mwisho cha huko Akhera. Hayo ni malipo yao kwa madhambi waliyo yafanya.
Ukirejea kutoka vitani wakawa baadhi ya hawa wanaafiki walio kataa kwenda vitani wakakutaka ruhusa watoke nawe kwenda Jihadi katika vita vingine, basi wewe usiwakubalie, na waambie: Hamtokwenda nami katika vita vyo vyote, wala hamtoshirikiana nami katika kupigana kokote na adui. Kwani kukaa kwenu nyuma msitoke pale mara ya kwanza hakukuwa na udhuru wowote unao faa, wala haikutokea toba yoyote ya kustahiki msamaha! Basi kaeni kama mlivyo ridhia kukaa pamoja na wazee na wakongwe na wanawake na watoto wadogo walio bakia nyuma.
Na akifa yeyote katika wao, basi usimsalie, wala usisimame kaburini kwake anapo zikwa, kwa sababu hawa wameishi maisha yao nao wakimkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wao wamekufa, nao wametoka katika Dini ya Mwenyezi Mungu.
Wala usistaajabu, ewe Mtume, kuona tulivyo wapa mali na wana, juu ya kuwa tumeudhika nao. Hayakuwa hayo kwa kuwa tunawapendelea wao zaidi, lakini ni kutekeleza anayo yataka Mwenyezi Mungu yawapate, nayo ni shakawa ya duniani kwa kushughulikia kukusanya mijimali tu pamoja na yaliyo lazimikana nayo. Nayo ni hizo hamu na masaibu yanayo ambatana na ukusanyaji wa mali. Na ili yatimie anayo yataka Mwenyezi Mungu yawe, nayo ni kuwa waifariki dunia nao ni makafiri, iwe wamekhasiri dunia na Akhera.
Na hawa wanaafiki wakisikia chochote ulicho teremshiwa katika Qur'ani kinacho wataka wamsafie Imani Mwenyezi Mungu, na wende kwenye Jihadi pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, matajiri na wenye nguvu katika wao wanakutaka uwaachilie wasende nawe kwenye Jihadi, na husema: Tuache tuwe na hawa walio pewa ruhusa kukaa nyuma Madina.