Haramu kwenu kuoa wake za watu wote, waungwana na wasio waungwana, ila mateka mlio wateka katika vita baina yenu na makafiri. Kwani ndoa zao zilizo pita zinafutika kwa kutekwa. Wanakuwa halali kwenu baada ya kuhakikisha hawana mimba. Basi shikeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu kuhishimu mlicho katazwa. Isipo kuwa hao wanawake Waumini walio maharimu yenu, mwaweza kutafuta wanawake mkawaoa kwa mali yenu, bila ya kuzini au kuweka kinyumba. Kila mwanamke mliye starehe naye baada ya kumwoa mpeni mahari yake kama mlivyo patana. Hapana ubaya kwenu ikiwa watakuridhieni kupunguza au kuongeza. Mwenyezi Mungu daima anayaangalia mambo ya waja wake, na ni mwenye kuwapangia hukumu zinazo wasilihi kwa maisha yao.
Asiye weza kati yenu kuwaoa wanawake Waumini wa kiungwana basi na aowe anaye muweza katika wanawake Waumini walio milikiwa. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema ukweli wa Imani yenu na ikhlasi yenu. Wala msione uvunjifu kuwaowa hao vijakazi, kwani nyinyi na wao ni sawa katika Dini. Basi waoweni kwa idhini ya watu wao, na muwape mahari yao mliyo wakadiria kwa mujibu ya ilivyo zowewa kati yenu kwa ajili ya kutendeana mema na kutimiza haki. Na chagueni wanawake walio safi, msichague wazinifu kwa dhaahiri wala mahawara wa kinyumba. Na hao wakija zini baada ya kuolewa basi adabu yao ni nusu ya muungwana. Na huku kuhalalishiwa kuowa wajakazi mnapo kuwa hamuwezi kunajuzu kwa anaye ogopa taabu zinazo pelekea zina. Na mkisubiri kuto owa wajakazi na mkakaa safi ni bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, na Mkubwa wa kurehemu.
Mwenyezi Mungu anataka kukuwekeeni wazi njia yenye maslaha kabisa, na akuongoeni kwenye nyendo njema za walio kuwa kabla yenu, na akurejesheni kwenye njia ya ut'iifu wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua vyema mambo yenu, ni Mwenye kupanga baraabara katika hukumu zake kwa yanayo silihi mambo yenu.