Enyi Waumini! Bila ya shaka katika Ibrahim na walio kuwa pamoja naye, kipo kiigizo kizuri kwenu kwa vile walivyo wafanyia uadui maadui wa Mwenyezi Mungu. Kiigizo hicho ni kwa mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kupuuza kufuata haya basi kajidhulumu nafsi yake. Kwani hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa mwenginewe. Yeye ni Mwenye kustahiki peke yake sifa zote njema.
Asaa Mwenyezi Mungu akajaalia yawepo mapenzi baina yenu na hao makafiri walio ni maadui zenu, kwa kuwapa tawfiki, kuwawezesha, kuingia katika Imani. Na Mwenyezi Mungu ana uweza ulio timia, ni Mkunjufu wa maghfira kwa mwenye kutubu, ni Mwenye kuwarehemu waja wake.
Mwenyezi Mungu hakukatazini kwa makafiri wasio kupigeni vita wala kukufukuzeni makwenu kuwakirimu na kuwapa mawasiliano mema. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda watu watendao ihsani na mawasiliano.
Ila Mwenyezi Mungu anakukatazeni wale walio kupigeni vita katika Dini ili kukuzuieni nayo, na wakakulazimisheni kutoka majumbani kwenu na nchi yenu, na wakasaidia katika kukutoeni huko, msiwafanye hao kuwa ndio wenzenu wa kusaidiana nao. Na wenye kuwafanya hao ndio wasaidizi wao, basi hao ndio wenye kujidhulumu nafsi zao.
Enyi mlio amini! Wakikujieni wanawake Waumini walio hama kukimbia nchi ya ukafiri, basi wachungueni ili mpate kujua ukweli wa Imani yao. Mwenyezi Mungu anajua zaidi ukweli wa Imani yao. Mkiwaona kama ni Waumini, basi msiwarudishe kwa waume zao makafiri. Wanawake Waumini si halali kwa makafiri, wala wanaume makafiri si halali kwa wanawake Waumini. Na wapeni waume wa kikafiri mahari waliyo yatoa kwa wake zao walio hamia kwenu. Wala hapana ubaya kwenu kuwaoa wanawake hao walio hamia kwenu mkiwapa mahari yao. Wala msiwazuie kwa kifungo cha ndoa wanawake makafiri walio bakia katika mji wa ukafiri au walio fungamana nao. Na takeni kwa makafiri mahari mliyo yatoa kwa wenye kufungamana na mji wa ukafiri. Na wao hao watake kulipwa walicho toa kuwapa wake zao walio hama wakaja kwenu. Hukumu hiyo ni kwa mujibu wa sharia ya Mwenyezi Mungu, anayo kufafanulieni. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema maslaha ya waja wake, ni Mwenye hikima katika kutoa sharia.
Na wakitokea baadhi ya wake zenu wakakukimbieni kwenda kwa makafiri, kisha mkapigana nao vita, basi wapeni walio kimbiwa na wake zao kiasi cha mahari waliyo yatoa. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.