Ni juu ya kina mama kuwanyonyesha wana wao muda wa miaka miwili iliyo timia kwa maslaha ya mtoto mchanga, akitaka hayo mmojapo au wote kati ya wazazi. Itamlazimu baba, kwa kuwa mtoto ni wake, amkimu mama kwa chakula na nguo kwa uwezo wake bila ya israfu wala uchoyo. Kwani haimlazimu mtu kufanya ila kiasi ya uwezo wake, na wala haitakikani kumletea madhara mama kwa kumnyima haki yake ya kumkimu yeye na kumlea mwana. Kadhaalika haitakikani mtoto awe sababu ya kumletea madhara baba yake kwa kumkalifu zaidi kuliko uwezo wake, au kumharimisha haki yake kwa mwanawe. Na akifa baba au akawa fakiri hawezi kazi kiamu kitakuwa juu ya mrithi wa mtoto ikiwa mtoto ana mali yake. Wakitaka wazazi kumwachisha ziwa mtoto kabla ya kutimia miaka miwili wakakubaliana kwa hayo na huku wakiangalia maslaha ya mtoto basi hapana ubaya. Na nyinyi wazazi mkitaka kumpa mama mwingine kumnyonyesha mtoto pia hapana ubaya - na hapo mtamtolea ujira kwa ridhaa na ihsani. Katika myatendayo muangalieni Mwenyezi Mungu, na mjue kuwa Yeye anayajua myatendayo na atakulipeni kwayo. Qur'ani inawajibisha mama amnyonyeshe mwanawe na asinyonyeshwe na mwingine ila kwa dharura, kwani kunyonyesha yeye ni faida kwa mama na mtoto katika siha. Na kuachisha ziwa kuwe kwa taratibu, na yajuzu kabla ya kutimiza muda ikiwa siha ya mtoto inaruhusu hayo