Katika mitindo ya watu ni kuwa pale tunapo waneemesha baada ya kwisha patwa na shida katika nafsi zao, au ahli zao (watu wao), au mali zao, hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema anazo waneemesha na kuwaondolea madhara. Bali huyakaabili hayo kwa kukakamia katika kuzikadhibisha na kuzikataa Ishara za Mwenyezi Mungu! Ewe Mtume! Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kukuhilikini na kukuadhibuni upesi upesi, lau kuwa si hukumu yake tangu hapo kukupeni muhula mpaka siku ya miadi aliyo iweka mwenyewe kwa ilimu yake peke yake. Hakika Wajumbe wetu, Malaika waliyo wakilishwa juu yenu wanaviandika vitimbi mnavyo vipanga, na Yeye Mwenyezi Mungu atakuhisabieni na atakulipeni.
Mwenyezi Mungu mnaye ikufuru neema yake, na mnakanusha Ishara zake, ndiye Yeye anaye kuezesheni kwenda na kutembea nchi kavu kwa miguu au kwa vipando, na baharini kwa vyombo alivyo fanya vikutumikieni, vinavyo kwenda juu ya maji, kama anavyo visahilishia Mwenyezi Mungu kwa upepo mzuri unao puliza kwa amani mpaka kufikilia huko vyendako. Hata mkisha tumaini na mkafurahia huvuma tena upepo mkali ukatibua mawimbi kutoka kila upande, na mkayakinika kuwa hapana ila kuhiliki tu! Katika shida kama hii hamna tegemeo ila Mwenyezi Mungu. Hapo basi mnamwomba madua kwa usafi wa niya, kwa kuyakinika kuwa hapana mwokozi isipo kuwa Yeye, na mnampa ahadi kuwa pindi akikuvueni na balaa hiyo mtamuamini, na mtakuwa wenye kushukuru.
Na akisha waokoa kutokana na khatari ya kuteketea, wanavunja ahadi yao, na mara wanarejea kwenye fisadi walizo kuwa nazo kabla! Enyi watu mvunjao ahadi! Hakika matokeo ya kupindukia mipaka ya starehe na kudhulumu kwenu yatarejea juu yenu peke yenu. Na hakika hizo starehe mnazo zistarehea katika dunia yenu ni starehe za kidunia zenye mwisho. Kisha marejeo yenu ya mwisho ni kwa Mwenyezi Mungu, na Yeye atakulipeni kwa vitendo vyenu mlivyo vitanguliza duniani.
Hakika hali ya uhai wa dunia kwa uzuri wake na starehe zake, na kisha baada ya hayo kutoweka, si chochote ila ni kama hali ya maji yanayo teremka mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi inayo liwa na watu na wanyama. Mimea hiyo ikastawi na ikatoa matunda, na ardhi ikapambika kwa kunawiri. Uzuri huo ukisha fika ukomo wake, na wenyewe wakayakinika kuwa kweli ni mali yao, na kuwa watanafiika kwa matunda yake na neema zake, amri yetu ya kuondoa yote hayo ikaja. Tukaifanya kama kwamba iliyo fyekwa, na kama kwamba haijapata kukaliwa wala haikupata kuwa na uzuri kabla yake! Na hali zote mbili za kustawi na kunawiri ya kufurahia watu na kinyume cha hayo, ni mambo ya kuondoka na kutoweka! Na kama alivyo bainisha Mwenyezi Mungu kwa mifano iliyo wazi, anabainisha Aya zake na anafafanua hukumu zake na Ishara kwa watu wanao fikiri na wanapima kwa akili. Aya hii inaashiria ukweli ulio anza kuchomoza, nao ni kuwa mwanaadamu kwa kuifanya ilimu imtumikie ameweza kuyamiliki anayo yataka. Hata inapo kuwa karibu ya kufikilia ukweli huu kukamilika, na akaona huyo mwanaadamu amekwisha fikilia kilele cha ujuzi, hapo basi amri ya Mwenyezi Mungu hutokea.
Na Mwenyezi Mungu anawaitia waja wake kwa Imani na vitendo vyema wendee Peponi, makao ya amani na utulivu. Na Yeye Subhanahu humwongoa amtakaye - kwa kuwa kesha jitayarisha vyema na kaelekea kheri - kwenye Njia ya Haki, nayo ni ya Salama.