Nabii Muhammad (s.a.w.) katolewa Makka na kalazimishwa kuihama kwa sababu ya vitimbi vya mapagani, washirikina, na kwa kuazimia kwao kumuuwa, ili Waislamu wapate kuwa na dola yao. Naye akenda kukaa Madina kwenye amani na manusura. Huko ikawa hapana budi ila kuwania kujilinda na uvamizi wa maadui, wasije wenye Imani wakapata mateso. Vikatokea hivyo Vita vya Badri. Waumini wakapata ushindi ulio wazi na ngawira nyingi waliziteka. Ikatokea khitilafu kidogo na suala katika shauri la ugawaji wa hizo ngawira. Ndio hivyo Mwenyezi Mungu anasema: Wanakuuliza khabari ya ngawira, zende wapi? Apewe nani? Ni za nani? Zigawanywe vipi? Ewe Nabii! Waambie: Hizo ngawira ni za Mwenyezi Mungu kwanza. Na Mtume, kwa amri ya Mola wake Mlezi, ndiye mwenye madaraka ya kuzigawa. Basi wacheni kukhitalifiana kwa ajili ya hayo. Na uwe mtindo wenu ni kumkhofu Mwenyezi Mungu na kumt'ii. Na tengenezeni yaliyo baina yenu, na mfanye mapenzi na uadilifu ndio makhusiano baina yenu. Kwani hakika hizi ndizo sifa za watu wa Imani.
Ama hakika Waumini wa haki na kweli daima wanakuwa na khofu na ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu. Akitajwa Allah Subhanahu, Mwenyezi Mungu Aliye takasika, nyoyo zao hufazaika, na zikajaa khofu. Kwa hivyo kila wakisomewa Aya za Qur'ani Imani yao inazidi kuwa imara, na wao huzidi unyenyekevu na ujuzi, na wala hawamtegemei yeyote ila Mwenyezi Mungu aliye waumba, na ndiye anaye walinda na kuwaendeleza.
Na hao Waumini walio wa kweli katika Imani, wanashika Swala kwa kutimiza nguzo zake, na kukamilisha unyenyekevu na ut'iifu, ili wawe daima katika kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na wanatoa katika mali aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, kwa ajili ya Jihadi, na mambo yote ya kheri, na kuwasaidia wanyonge.
Hakika hawa wanao sifika kwa sifa hizi ndio khasa wanao sifika kwa Imani kwa haki na kweli. Na malipo yao ni kupata vyeo vya ngazi ya juu kwa Mwenyezi Mungu. Yeye Allah Subhanahu ndiye ataye wapa radhi zake, na maghafira wanapo teleza, na duniani atawapa riziki njema, na Akhera neema ya daima.
Ushindi, bila ya shaka, upo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Na funguo za mambo yote ziko kwake. Na hali ya Waumini katika kukhitalifiana kwao katika mambo ya ngawira ni kama hali yao pale alipo kuamrisha Mwenyezi Mungu utoke ukapigane na washirikina katika Badri, nayo ni Haki iliyo thibiti. Kwani miongoni mwa Waumini kulikuwapo na kikundi kilicho chukia vita kweli kweli.
Wanajadiliana nawe hao wa kikundi hicho, na wanajaribu kutilia nguvu kauli yao katika jambo la haki, nalo ni kutoka kwa ajili ya Jihadi. Na kumbe wao walikuwa na wenzao walio toka kwenda kupokonya mali ya Makureshi yaliyo kuwa yanakwenda Sham, na wasiyapate. Kikundi hichi kikakhiari kurejea baada ya kuona wamenusurika, kwa kujuvywa na Mtume, na kwamba makafiri wanawaogopa, na kwa kuwa hadi wakivichukia vita, na kuwa hawajui litalo wapata. Na walipo kuwa wakiviendea vita walikuwa kama wanao sukumwa kwenda kufa, na wao wanaona kitacho wauwa, na yanawapata mateso yake.
Enyi Waumini! Kumbukeni ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenu kwamba atakupeni ushindi juu ya moja katika makundi mawili, hilo lenye silaha na nguvu. Na hali nyinyi mnapendelea kupambana na hilo kundi jengine lenye mali na watu tu. Na hilo ni msafara wa Abu Sufyan. Nanyi mkakhiari mali yasiyo kuwa na wapiganaji. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka kuithibitisha Haki kwa mapendo yake na uwezo wake na kwa maneno yake yaliyo kwisha tangazwa, na ili aung'oe kabisa ukafiri katika Bara Arabu kwa ushindi wa Waumini. Aya hizi tukufu zinatoa sura ya yanayo pita katika nafsi wakati wa vita, nako ni kutamani kukutana na maadui wachache na kuchukia kukutana na wengi, na kupenda kuteka mali na ngawira; na ilhali Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka kuitukuza Dini na ishinde Haki na wang'oke makafiri.
Ili athibitishe Haki, na auondoe upotovu, hata wakichukia makafiri ambao wamedhulumu Haki ya Mwenyezi Mungu na Haki ya Waumini na Haki ya nafsi zao wenyewe.