Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni kuvua wanyama wa baharini, na muwale, na wanufaike kwao wakaazi wenyeji na wasafiri. Na amekuharimishieni kuwinda wanyama wa bara wasio fugwa kwa kawaida majumbani, katika muda ule unapo kuwa katika Hija au Umra, kwenye eneo takatifu linalo itwa Alharam. Na mzingatieni Mwenyezi Mungu, na iogopeni adhabu yake. Basi msende kinyume naye, kwani nyinyi mtarejea kwake Siku ya Kiyama, na hapo atakulipeni kwa yote mliyo yatenda. (Huu ni mfano katika mifano mingi ya Uislamu tangu hapo kale unavyo pendelea kulinda tabia ya mazingara kwa kuhifadhi wanyama wasiuliwe ovyo, na miti isikatwe ovyo, na hata maji ya mito na maziwa yasitumiwe kwa fujo, kwani Mwenyezi Mungu hawapendi wafujaji!)
Mwenyezi Mungu ameijaalia Al Kaaba, nayo ni hiyo nyumba aliyo itukuza na akaharimisha watu na wanyama kufanyiwa uadui ndani yake na karibu yake, ameijaalia kuwa yenye kusimama na yenye kutukuzwa, na yenye kuwapa amani watu, na iwe ndiyo Kibla cha kuelekea watu katika Swala zao, na watu waiendee kwa Hija wawe ni wageni wa Mwenyezi Mungu, na ili watende yale ya kuupa nguvu umoja wao. Hali kadhaalika ameufanya mwezi wa Hija na wanyama wanao tolewa dhabihu, na khasa wale wanao vishwa vigwe ili watambuliwe na wanao waona kuwa hao wametolewa hidaya kwenye hiyo Nyumba. Na natija ya kuweka yote hayo ni kuwa mpate kuyakinika kuwa ujuzi wake Mwenyezi Mungu umeenea kila kitu kilioko mbinguni kunakotoka wahyi (ufunuo) wa sharia, na umeenea duniani, anako weka sharia ya kuwaletea watu maslaha yao. Na hakika ujuzi wa Mwenyezi Mungu umeenea juu ya kila kitu.
Enyi watu! Jueni kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali, humteremkia anaye halalisha vya haramu, naye pia ni Mwingi wa kusamehe dhambi za mwenye kutubu na akaingia kumt'ii. Naye ni Mwenye rehema sana, na kwa hivyo hamchukulii mtu papo kwa papo kwa kila alitendalo.
Haimlazimikii Mtume ila kuwafikishia watu anayo funuliwa yeye, ili isimame hoja juu yao na wasiwe na kisingizio chochote cha kuwa ati hawakuonywa wala hawakufunzwa. Basi yajueni anayo kuleteeni Mtume, kwani Mwenyezi Mungu anayajua mnayo dhihirisha na mnayo yaficha.
Ewe Nabii! Waambie watu: Si sawa sawa vile vizuri anavyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu na vibaya anavyo kuharimishieni. Kwani farka iliyo baina ya viwili hivyo kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa, na hata hivyo vibaya vingawa ni vingi na vinawapendeza watu wengi. Basi enyi wenye akili! Ufanyeni ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu uwe ni kinga yenu isikupateni adhabu yake kwa kukhiari vilivyo vyema, na kujiepusha na viovu, ili mpate kuwa miongoni walio fuzu duniani na Akhera.
Enyi mlio amini! Msimuulize Nabii mambo ambayo Mwenyezi Mungu amekuficheni mkataka yafichuliwe, na mkamuuliza Nabii katika uhai wake, kwani Qur'ani inamteremkia bado. Na Mwenyezi Mungu atakubainishieni itapo hitajika. Mwenyezi Mungu amekusameheni kwa yasiyo tajwa, hatokuadhibuni kwayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, na Mwenye wasaa katika upole. Basi hana papara katika kuadhibu.
Katika jamaa walio kutangulieni walikuwapo walio uliza mfano wa haya, mambo mazito mazito; na Manabii wao walipo wakalifisha ya kufanya wakaona mazito kuyatenda, wakayaacha, na wakawa ni wenye kuyakanya. Kwani Mwenyezi Mungu hupendelea wepesi, wala hapendelei uzito; na huwakalifisha watu kwa wanayo yaweza.
Mwenyezi Mungu hakukupeni ruhusa kuharimisha kitu alicho kuhalalishieni, na kwa hivyo mkenda mkawapasua ngamia masikio yao, na mkajizuia kuwatumia mkawaita "Bahira" mkawawacha kwa kuwekea nadhiri, na mkawaita "Saiba"; na mkaharimisha kula kondoo dume, na mkawatoa kuwa tunza kwa masanamu; na hata kondoo akizaa dume na jike mkamwita "Wasila", na mkakataa kumchinja dume lake. Wala Mwenyezi Mungu hakukufanyieni sharia ya kukuharimishieni msimtumie ngamia dume baada wakisha zalikana kutokana naye matumbo kumi, naye mkamwita "Hami"! Mwenyezi Mungu hakukutungieni sharia yoyote ya namna hiyo. Lakini walio kufuru wanazua uwongo na wanamsingizia Mwenyezi Mungu. Na wengi wao hawatumii akili. Wakati wa Jahiliya, kabla ya Uislamu, Waarabu wakijiharimshia wenyewe asiyo yaharimisha Mwenyezi Mungu. Katika hizo ni kuwa:- 1. Ngamia akizaa mara tano na mtoto wa mwisho akawa dume, basi wakimpasua sikio lake na wakaharimisha kumpanda, na akawa haijuzu kumfukuza kwenye kunywa maji au kula machunga. Na wakimwita: "Bahira", yaani aliyepasuliwa sikio. 2. Ilikuwa mtu husema: Nikirejea safarini, au nikipona maradhi yangu, basi ngamia wangu ni "Saiba", yaani aliye achwa, na anakuwa kama "Bahira". 3. Na walikuwa kondoo akizaa jike humfanya huyo mtoto ni wao, na akizaa dume humfanya ni wa miungu yao; na akizaa dume na jike basi hawamtoi mhanga huyo dume tena kwa miungu yao, na humwita huyo kondoo jike: "Wa'sila", yaani amemuwasilia nduguye dume. 4. Na pia walikuwa akitokana na fahali mizao kumi basi husema mgongo wake umehamika,yaani umehifadhika, na wakamwita "Hami". Huwa basi hapandwi, wala hatwikiwi mizigo.