Walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakawazuilia watu wasiingie katika Uislamu, Mwenyezi Mungu amevivunja vyote walivyo vitenda.
Na walio amini, na wakatenda mema, na wakasadiki yaliyo teremshwa kwa Muhammad, nayo ni Haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, atawafutia makosa yao, na atawatengenezea hali yao ya Dini na dunia.
Hayo ni kwa sababu walio kufuru wamefuata njia ya upotovu, na kwamba walio amini wamefuata njia ya Haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi. Kwa mfano kama huu wa kubainisha kwa uwazi ndio Mwenyezi Mungu anawaeleza watu hali zao ili wapate kuzingatia.
Mtapo kutana na walio kufuru katika vita basi wapigeni kwenye shingo zao, mpaka mtakapo wadhoofisha kwa wingi wa kuwauwa, basi tena wafungeni mateka. Tena ama waachilieni wende zao kwa wema na ihsani, baada ya kwisha vita, kwa kuwaachia bila ya fidia, au kwa fidia ya kutoa mali au kubadilishana kwa mateka wa Kiislamu. Inakuwa mmewaachilia kwa badali. Huu ndio uwe mwendo wenu na makafiri mpaka vita vimalizike kabisa. Mwenyezi Mungu anawahukumieni hivyo. Na lau angeli taka bila ya shaka angeli washinda bila ya vita, lakini haya ni ili awajaribu Waumini kwa makafiri kama mtihani ndio ameamrisha Jihadi. Na walio uwawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kabisa hatoacha vitendo vyao vipotee. Atawahidi, na azitengeneze nyoyo zao, na awatie katika Pepo aliyo kwisha wajuulisha. Katika Aya hii tukufu zimetajwa "shingo" khasa, kwa sababu kuzipiga hizo ndio njia inayo faa mno kummaliza upesi mwenye kupigwa bila ya kumuadhibu na kumtesa. Kwani imethibiti kwa ilimu kuwa shingo ndiyo kiungo baina ya kichwa na kiwiliwili kizima. Basi ukikatika mshipa wa uti wa mgongo wenye kupeleka hisiya zote, basi viungo vyote muhimu vinapooza. Na ikikatika mishipa ya damu, damu inasita kufika kwenye ubongo. Na zikikatika njia za kupitisha hewa, basi pumzi husita. Na katika hali hizi zote uhai unakatika mara moja.
Enyi mlio amini! Mkiinusuru Dini ya Mwenyezi Mungu, na Yeye atakunusuruni muwashinde maadui zenu, na ayatilie nguvu mambo yenu.
Mambo yao ni hivyo kwa sababu wao wanakereka na aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, yaani Qur'ani na amri zake. Basi Mwenyezi Mungu amevibat'ilisha vitendo vyao.
Wameshindwa kutafuta ya kuwazindua, hata hawakutembea katika ardhi wakaangalia hali gani ulikuwa mwisho wa walio wakadhibisha Mitume kabla yao? Mwenyezi Mungu aliwateremshia hilaki katika kila kilicho khusiana nao, nafsi zao, mali yao, na watoto wao. Na wenye kumkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake ndio hupata mwisho mfano wa huo.
Malipo hayo ndio ushindi wa Waumini na kushindwa nguvu makafiri, ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ni rafiki mlinzi wa walio amini na ndiye Mwenye kuwanusuru; na makafiri hawana rafiki mlinzi wa kuwanusuru wala kuwakinga na kuangamia.