Hawato huzunishwa na Kitisho Kikubwa kinacho wafazaisha makafiri. Na Malaika watawapokea kwa kuwapongeza kwa kusema: Hii ndiyo Siku yenu ya neema aliyo kuahidini Mola wenu Mlezi!
Siku tutapo zikunja mbingu kama zinavyo kunjwa karatasi katika kitabu. Na tutawarejeza viumbe kwa ajili ya hisabu na malipo. Wala hatushindwi kuwarejeza, kwani tuliwaumba mara ya kwanza. Na kama tulivyo waanza tutawarejeza. Ahadi yetu kwa hayo ni ahadi ya kweli. Daima Sisi tunatenda tunayo yaahidi.
Na tulikwisha andika katika Zaburi - nacho ni Kitabu cha Daud baada ya Taurati - kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema wapate kuitengeza, na kusahilisha njia za maisha bora humo. ("Bali wenye upole watairithi nchi"..Zaburi 37.11 "Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele".. Zaburi 37.29)
Hakika katika haya tuliyo yataja, khabari za Manabii pamoja na kaumu zao, na khabari za Pepo na Moto, yanatosha kuwakumbusha na kuwafanya wazingatie watu walio tayari kumuabudu Mwenyezi Mungu pekee na hawasalitiki na mapambo ya dunia.
Ewe Nabii! Sema: Hakika kiini cha Wahyi aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni kwamba hakika nyinyi hamna Mungu isipo kuwa Yeye. Na yote yaliyo bakia niliyo funuliwa yanafuata asili hii. Ikiwa mambo ni hivyo, basi inakuwajibikieni mjisalimishe na mnyenyekee kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Wakito ujali wito wako, basi waambie: Nimekufunzeni yote aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi; na kwa hivyo tumekuwa sawa kwa kuyajua hayo. Wala mimi sijui hayo ya kufufuliwa na kuhisabiwa mliyo ahidiwa, yatakuwa karibu au mbali.
Na sijui pengine huko kupewa muhula na kuakhirishiwa adhabu nyinyi ndio Mwenyezi Mungu anakufanyieni mtihani tu, na kukustarehesheni kwa ladha za maisha mpaka alipo kadiria Mwenyezi Mungu kukuhisabieni kwa hikima yake.
Ewe Nabii! Sema: Ewe Mola Mlezi! Tuhukumu baina yangu na hawa nilio wafikishia Wahyi kwa uadilifu ili wasiwe sawa Waumini na makafiri. Na Mola wetu Mlezi Mwenye kuneemesha kwa neema kubwa, Mwenye kustahiki kuhimidiwa na kushukuriwa, ndiye wa kutakiwa msaada kuvunja uzushi mnao zua, enyi makafiri.