Hakika walio ongoka na walio potoka hawawi sawa. Basi je, anaye jua ya kuwa uliyo teremshiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliye kulea akakuumba akakuteuwa kufikisha ujumbe wake, kuwa ni Haki isiyo na shaka yoyote...je huweza kuwa huyo kama aliye potea akaitupa Haki, hata akawa kama kipofu? Hakika hawatambui Haki wakazingatia utukufu wa Mwenyezi Mungu, ila watu wenye akili ya kufikiri.
Hao ndio wanao tambua Haki. Wao ndio wanao timiza ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyo juu yao kwa muujibu wa maumbile, na kwa muujibu wa maagano yao na ahadi zao walizo fungamana nazo; wala hawavunji maagano walio fungamana nayo kwa jina la Mwenyezi Mungu baina yao na waja wenzi wao, na kwa maagano makubwa walio jifunga nayo kwa maumbile yaliyo wafanya waitambue Haki na waamini, isipo kuwa walipo jipoteza wenyewe nafsi zao.
Hao ni Waumini; ada yao ni mapenzi na ut'iifu. Hao wanaamini mapendo baina ya watu, na wanahurumia jamaa zao, na wanawasaidia wenzi wao katika Haki, na wao wanaijua Haki ya Mwenyezi Mungu, na wanaiogopa hisabu ya kuwachusha Siku ya Kiyama, na kwa hivyo wanajikinga na madhambi kwa kadri wawezavyo.
Na wanavumilia maudhi wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu iwasaidie katika Njia ya kuwania Haki. Wanashika Swala kama inavyo pasa kusafisha roho zao, na kumkumbuka Mola wao Mlezi. Na wanatoa kutokana na mali aliyo wapa Mwenyezi Mungu kisirisiri na kwa dhahiri bila ya kutaka kuonyesha watu, na kwa maovu wanao tendewa wao wanalipa mema. Na wao kwa sifa hizi watapata malipo mema kwa kukaa katika ahsani ya nyumba, nayo ndiyo Pepo.
Hayo ndiyo malipo mema, ya ukaazi wa moja kwa moja katika Bustani za neema. Watakuwa wao humo pamoja na wazazi wao walio kuwa njema Imani yao na a'mali yao. Pamoja nao pia watakuwa na wake zao na dhuriya zao (wazao wao). Na Roho Safi zitawasalimu na kuwaingilia kila upande.
Hizo Roho zitawaambia: Amani ya milele ni yenu kwa sababu ya kuvumilia kwenu maudhi, na kusubiri kwenu katika kupambana na matamanio yenu. Ni mazuri mno haya malipo mnayo yapata, nayo ni kupata makaazi katika Nyumba ya Neema ya Peponi.
Hakika sifa za Waumini wema ni kinyume na sifa za washirikina waovu. Kwani washirikina huvunja ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo chukua kwao kwa mujibu wa maumbile na ambayo walijifunga nayo. Kwa hivyo wamekhalifu maumbile yao na akili zao kwa kuabudu mawe yasiyo wafaa wala kuwadhuru. Na wanavunja ahadi zao wanazo fungamana na waja wenzao, tena wanakata makhusiano yao ya mapenzi na watu, na makhusiano yao na Mwenyezi Mungu. Hawazifuati amri zake, wala hawamuabudu Yeye pekee. Na wanafanya uharibifu katika ardhi kwa uvamizi na kufanya uadui na kuvuka mipaka, na kuacha kuitengeneza dunia wakanafiika nayo! Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika hapendi uchafuzi na ufisadi.
Na ikiwa hao washirikina wanaona kuwa wao wamepewa mali mengi, na Waumini ni mafakiri, wanyonge, basi wajue kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu humpa riziki kunjufu amtakaye akizishika sababu na humdhikisha amtakaye. Basi Yeye humpa Muumini na asiye kuwa Muumini. Kwa hivyo msidhani kuwa wingi wa mali mikononi mwao kuwa ni dalili ya kuwa wao ndio wamo katika Haki. Lakini wao hufurahi kwa hayo mali walio pewa, juu ya kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu humpa dunia anaye mpenda na asiye mpenda. Na maisha ya duniani si chochote ila ni starehe duni yenye kupita!
Na hakika hao washirikina walio banwa na wingi wa pupa na papara husema: Je, huyu Nabii hakuteremshiwa muujiza mwengine kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Ewe Nabii! Waambie: Sababu ya kutokuwa na Imani nyinyi si upungufu wa miujiza, bali ni upotovu tu! Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka humwacha apotee anaye mtaka apotee, maadamu anaendelea katika njia ya upotovu. Na humwongoa aendee kwenye Haki yule ambae daima hurejea kwa Mwenyezi Mungu.
Na hakika hawa wanao rejea kwa Mwenyezi Mungu, na wanaikubali Haki, ndio hao walio amini ambao nyoyo zao zinatua anapo tajwa na kukumbukwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Qur'ani au vyenginevyo. Na hakika nyoyo hazitulii na kutua ila kwa kukumbukwa utukufu wa Mwenyezi Mungu na uwezo wake na kuombwa radhi yake kwa kumt'ii.