Mwenyezi Mungu akasema: Dua zenu zimeitikiwa. Basi endeleeni katika Njia Iliyo Nyooka, na iwacheni njia ya wale wasio jua mambo yalivyo, wala hawaifuati Haki iliyo wazi.
Tulipo wavusha bahari Wana wa Israili, Firauni na askari wake waliwafuatia nyuma yao, tukawafunika kwa bahari! Alipo kuwa anazama, Firauni alisema: Nimemsadiki Allah, Mwenyezi Mungu, walio msadiki Wana wa Israili, na wakamfuata. Na mimi ni katika wenye kut'ii walio wanyenyekevu!
Mwenyezi Mungu hakukupokea kuamini huko kwa Firauni ambako alikuwa hana budi nako. Toba hiyo ilikuwa pale mauti yamekwisha mkabili, naye aliishi maisha yake yote katika kumuasi Mwenyezi Mungu, akifisidi nchi, naye akafa kafiri wa kutupwa!
Na leo siku ulipo angamia tutautoa mwili wako baharini, na tutauweka uwe ni onyo na funzo kwa hao walio kuwa wakikuabudu, na hawakuwa wakikutarajia utapata mwisho huu wa hizaya wa machungu. Lakini watu wengi wanaghafilika na Ishara zilizo wazi na zilizo zagaa katika ulimwengu, na ambazo zinathibitisha uwezo wetu. Inaonyesha Aya hii tukufu kuwa mwili wa Firauni utabaki umehifadhiwa ili watu wauone, na wapime kwa macho yao hali ya ule mzoga wa yule aliye kuwa akijiona ni mungu, na akiwaambia watu wake wanao mnyenyekea: Hamna mungu ila mimi! Kadhaalika tujue kuwa kutoka Wana wa Israili katika nchi ya Misri kulikuwa mwishoni mwa karne ya kumi na tatu kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s., katika enzi ya mmoja wa Mafirauni wa Ukoo wa kumi na tisa, naye ni Minfitah mwana wa Ramsis wa Pili, ambaye ndiye aliye wakandamiza Wana wa Israili akawalazimisha wamjengee Jiji la ufalme wake. Uvumbuzi wa machimbo ya vitu vya kale wa hivi karibuni umedhihirisha kuwa jina la mji huo ulio funikika chini ya ardhi, ni "Bur'amsis". Kulikuwa kutoka kwa Wana wa Israili pamoja na Musa ni kwa ajili ya wito wa Tawhidi, Umoja wa Mwenyezi Mungu, na kuikata shemere ya Firauni iliyo wadhalilisha, na ikawakutisha adhabu ya mwisho. Na ilikuwa haijuulikani na Waarabu ambao hawajui kusoma na kuandika, wala kwa wengineo, kwamba mwili wa Firauni huyu ungalipo mpaka hii leo. Lakini Qur'ani imeyataja hayo, na ukweli wake umethibiti mwaka 1900 B.K., yaani karne kumi na tatu baada ya kuteremka Qur'ani. Je, hii si dalili ya kuwa imetoka kwa Mungu?
Na tuliwaweka vyema Wana wa Israili wakaishi katika nchi nzuri na huku wakiihifadhi Dini yao, nao wako mbali na dhulma iliyo kuwa ikiwapata; riziki na neema zimewajalia. Lakini mara baada ya kuonja neema ya utukufu baada ya unyonge, yaliwasibu maradhi ya kufarikiana. Wakakhitalifiana juu ya kuwa imekwisha bainika kweli na uwongo! Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama, na atamlipa kila mmoja kwa alilo tenda.
Ikikuingia shaka wewe au mwengineo katika huu wahyi tuliyo kuteremshia, basi waulize watu wa Vitabu vilivyo tangulia walivyo teremshiwa Manabii wao. Kwao utapata jawabu ya kukata, yenye kuwafikiana na haya tuliyo kuteremshia wewe. Na hayo ni kutilia mkazo ukweli wa uwazi wa dalili pindi ikitokea shaka yoyote. Basi hapana njia ya kutia shaka. Sisi tumekuteremshia Haki isiyo na shaka yoyote. Basi usishindane na yeyote mwenginewe katika kutia shaka na kutaradadi.
Wala usiwe wewe, wala yeyote katika wanao kufuata, miongoni mwa wanao kadhibisha hoja na Ishara zilio wazi, msije mkaingia khasarani na ghadhabuni, kama hali ya makafiri wasio amini. Na akisemezwa Nabii basi ndio wanasemezwa wote wanao mfuata.
Hakika wale iliyo kwisha pita juu yao hukumu ya kuwa wao ni makafiri, kwa kujuulikana inadi yao na chuki zao, hawatoamini hata ukijihangaisha vipi nafsi yako kuwakinaisha.