Haimfalii Nabii yeyote kukamata mateka, au kuchukua fidia, au kutoa bure msamaha, mpaka ashinde, na maadui waone wameshindwa, na wawe wamepata pigo kubwa hata kuwa hawawezi tena kupigana katika nchi. Lakini, nyinyi jamaa wa Kiislamu, mmefanya haraka katika Vita vya Badri kukamata mateka kabla hamjatamakani mkawa imara katika nchi. Mnatafuta manufaa ya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera, kwa kutukuzwa Neno la Haki, na lisikushughulisheni la dunia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda. Hukupangieni mambo yenu kwa mujibu wa faida yenu.