Qur'ani imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu, ambaye hana wa kumshinda kwa atakayo; Mwenye hikima katika vitendo vyake na utungaji wa sharia zake.
Hakika Sisi tumekuteremshia wewe, Muhammad, Qur'ani hii yenye kuamrisha Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia ibada Yeye tu peke yake.
Jueni na mtambue kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye Dini isiyo kuwa na ila. Na washirikina walio wafanya wenginewe kuwa ni wasaidizi wa kuwanusuru, wanasema: Sisi hatuwaabudu hawa kwa kuwa ni waumbaji, bali tunawaabudu wapate kutukaribisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa mkaribisho wa kutuombea sisi kwake Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina ya hawa washirikina na Waumini wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja katika yale wanayo khitalifiana katika matatizo ya shirki na Tawhidi. Hakika Mwenyezi Mungu hamjaalii afikie Haki mtu ambaye mtindo wake ni uwongo na kukanya.
Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, kama wasemavyo Wakristo kwa Masihi, na washirikina kwa Malaika, basi angeli jichagulia amtakaye katika viumbe vyake, la sio kama mtakavyo nyinyi. Mwenyezi Mungu ametakasika na upungufu wa kuhitajia mwana. Yeye ni Mwenyezi Mungu asiye kuwa na mfano kama Yeye. Mtenda kama apendavyo, ukomo wa kutenda.
Ameumba mbingu na ardhi kwa kushikamana na Haki na kuwa sawa kwa kufuatana na sharia zilizo thibiti. Usiku unaufunika mchana, na mchana unaufunika usiku kwa mfululizo. Na amedhalilisha jua na mwezi kwa mujibu atakavyo na kwa mujibu wa maslaha ya waja wake. Kila kimojapo katika hivyo vinakwenda katika njia yake mpaka ufike wakati aliyo uwekea Yeye, nao ni Siku ya Kiyama. Jueni basi kuwa Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye kushinda kila kitu. Basi hapana kitu chochote kilicho tokana na atakavyo Yeye, ambaye amefikilia ukomo wa kuwasamehe wenye kutenda madhambi katika waja wake. Aya hii tukufu inaonyesha kuwa ardhi ina sura ya mviringo kama mpira, na inazunguka wenyewe kwa wenyewe juu ya msumari-kati wake. Kwani kule kutumiwa neno Yukawwiru katika Kiarabu na ikafasiriwa Hufunika, maana yake ni kufunika kitu kwa kitu kwa namna ya kufuatana, kukariri, mara kwa mara. Na lau kuwa ardhi haina sura ya mpira, kwa mfano kuwa batabata tu, usiku ungeli enea kote kwa ghafla, au mchana ungeli angaza dunia nzima kwa mara moja.