Hawakuwa walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake miongoni mwa Mayahudi na Wakristo, na miongoni mwa washirikina, waache kughafilika kwao na ujinga wao kuto ijua Haki mpaka iwajie hoja ya kukata.
Wala hawakufarikiana walio pewa Kitabu katika Mayahudi na Wakristo, ila baada ya kuwajia hiyo hoja iliyo wazi yenye kuonyesha ya kwamba Muhammad ndiye huyo Mtume wa Mwenyezi Mungu aliye ahidiwa katika Vitabu vyao.
Na hawakulazimishwa jambo katika walio lazimishwa ila iwe ibada yao kwa Mwenyezi Mungu ni kumsafia Yeye Dini, waache upotovu wasimame sawa kwenye Haki, na wazihifadhi Swala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Mila Iliyo Nyooka.
Hakika wale walio kufuru katika Watu wa Kitabu na washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu, wala hawatatoka humo. Hao ndio waovu wa viumbe kwa itikadi na vitendo.
Malipo yao Akhera kwa Imani na vitendo vyema walivyo vitanguliza, ni Mabustani ya kudumu yenye kupitiwa na mito kati yake, watakaa humo milele. Mwenyezi Mungu amepokea a'mali zao, na wao watamshukuru kwa hisani yake aliyo wafanyia. Hiyo ndiyo jaza ya mwenye kuiogopa adhabu ya Mola wake Mlezi, akaamini na akatenda mema.