Hakika Sisi tulimtuma Nuh'u kwa watu wake, na tukamwambia: Waonye watu wako kabla haijawajia adhabu yenye machungu makali.
Ndipo Mwenyezi Mungu atapo kusameheni madhambi yenu, na atakupeni umri mrefu mpaka ifike ajali iliyo wekwa mwisho wa umri wenu. Hakika mauti yakija hayaakhirishwi kabisa! Lau kuwa mngeli jua majuto mtakayo kuwa nayo utapo kwisha muda wenu mngeli amini.
Na mimi kila nikiwataka wakuamini Wewe upate kuwasamehe, hubandika vidole vyao kwenye masikio yao ili wasisikie wito wangu, na hujifunika kwa maguo yao ili wasiuone uso wangu! Na wakasimama kidete juu ya ukafiri wao, na wakatakabari kutakabari kukubwa mno!
Nikawambia watu wangu: Takeni kwa Mola wenu Mlezi maghfira kwa kufru zenu na maasi yenu. Kwani Yeye bado ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya mwenye kurejea kwake.
Na atakupeni mali na wana, na hayo ndiyo mapambo ya dunia, na atakupeni mashamba mtayo starehea kwa uzuri wake na matunda yake, na atakujaalieni mito ya kunyweshea mazao yenu na mifugo yenu.
Na akaufanya mwezi katika mbingu hizo unatoa nuru, na akalifanya jua ni taa ambayo kwayo watu wa duniani ndio wanaona kwa mwangaza wake yote wanayo hitajia kuyaona?
Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na ardhi, akakuotesheni kama miema kwa njia ya ajabu, kisha baada ya kufa atakurejesheni huko huko kwenye ardhi, na tena atakutoeni huko kwa hakika hapana hivi wala hivi.
Alisema Nuh'u: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikatalia mimi niliyo waamrisha ya kuamini na kutaka msamaha, na wakawafuata madhaifu miongoni mwao ambao mali yao na watoto wao hawawazidishii ila khasara tupu katika Akhera.
Na wao wakiwaambia: Msiache kuiabudu miungu yenu, wala msimwache Wadda, wala Suwaa' , wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra. Na hawa walikuwa miungu ya masanamu iliyo chongwa kwa sura ya wanyama namna mbali mbali.
Na miungu hii iliwapoteza watu wengi. Na wala huwazidishii wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na inda, ili kuzidi kubaidika na Haki.
Kwa sababu ya madhambi yao wakazamishwa kwa tofani, na baada ya kuangamizwa kwao wakatiwa Motoni kwenye moto mkali wa kuwaka na kuteketeza, na wala wasipate yeyote baada ya kumkosa Mwenyezi Mungu, wa kuwanusuru na kuwakinga na adhabu!
Na Nuh'u akasema baada ya kukata tamaa nao watu wake: Mola wangu Mlezi! Usimwache yeyote katika hao wanao kukataa Wewe akabaki akizunguka juu ya ardhi!
Ewe Mola wangu Mlezi! Ukiwaacha hao bila ya kuwateketeza na kuwang'oa watawatia waja wako katika upotovu, na wao hawatozaa ila wenye kupotoka vile vile wakaiacha haki, na wakakithiri kukukanya na kukuasi.
Mola wangu Mlezi! Nisamehe mimi na wazazi wangu ambao ndio walio kuwa ni sababu ya kuzaliwa mimi, na kila mwenye kuingia nyumbani kwangu kwa kukuamini Wewe, na uwasamehe Waumini wote wanaume na wanawake. Na usiwazidishie makafiri ila kuwaangamiza.