Macho yao yatainamia chini kwa wingi wa kitisho, wakitoka makaburini kama kwamba ni nzige walio tawanyika, kwa wingi wao na mbio zao.
Wakimkimbilia huyo mwitaji, wakimtazama kwa unyonge na unyenekevu, macho yao yanamwangalia yeye tu. Makafiri watasema Siku ya Kiyama: Hii leo ni siku nzito, siku ya shida!
Kabla ya makafiri wa Makka walikwisha kanusha kaumu ya Nuhu. Walimkadhibisha Nuhu, mja wetu na Mtume wetu, wakamsingizia kuwa ana wazimu. Wakaingiza baina yake na kufikisha kwake Ujumbe kila namna ya maudhi na vitisho.
Na tukaipasua ardhi kwa chemchem zikitibuka maji. Yakakutana maji ya mbinguni na maji ya ardhi kuwahiliki, kama alivyo kadiria Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Wakasema: Hivyo aje mtu tu katika sisi, watu wa kawaida, asiye na watu, nasi tumfuate? Tukimfuata huyo basi bila ya shaka sisi tutakuwa mbali mno na haki, na tutakuwa tuna wazimu basi.
Uteremshiwe wahyi kwake yeye katika sisi na hali wapo wanao stahiki zaidi? Bali huyo kazikdi katika uwongo, mwenye kukanya neema.
Hakika Sisi tunampelekea Mtume wetu Saleh ngamia mke, awe ni mtihani wao. Basi wangojee, na uwatazame watafanya nini. Na subiri, uvumilie maudhi yao mpaka itapo kuja amri ya Mwenyezi Mungu.
Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao na ngamia. Kila mmoja wao atakuwa na zamu yake aje kunywa katika siku yake.
Sisi tuliwapatiliza kwa ukelele mmoja tu, wakawa kama miti mikavu anayo ikusanya yeyote atakaye kujengea boma la uwa wake.
Na bila ya shaka Sisi tumeisahilisha Qur'ani iwe nyepesi kwa ajili ya mawaidha na kuzingatia. Lakini je, yupo wa kuwaidhika?
Hakika Sisi tuliwapelekea upepo mkali wa kuwatupia changarawe. Isipo kuwa watu wa Lut'i walio amini. Hao tuliwaokoa na adhabu hii mwisho wa usiku.
Wakamtaka awape wageni wake wawatende fiili yao, tukayafuta macho yao kuwa ni malipo kwa hilo walilo litaka. Basi waambie kwa kuwakejeli: Igugumieni adhabu yangu, na maonyo yangu!
Walikadhibisha Ishara zetu na miujiza yetu waliyo kuja nayo Mitume wetu. Tukawaangamiza kwa maangamizo ya nguvu yasiyo shindika, ya uwezo mkubwa.
Ati nyinyi, makafiri, mna nguvu zaidi kuliko hao wa kaumu zilizo tangulia ambao wameangamizwa? Au nyinyi mmetolewa makosani kwa ilivyo teremka katika Vitabu vya mbinguni?