Dhul-Qarnaini alipo kwisha jenga ile ngome alisema kumshukuru Mwenyezi Mungu: Ngome hii ni rehema iliyo toka kwa Mola wangu Mlezi kwa ajili ya waja wake. Na itabaki hivi hivi imesimama mpaka ije amri ya Mwenyezi Mungu kuiteketeza. Hapo tena itakuwa sawa sawa na ardhi. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima itimie bila ya muhali.
Na tangu kujengwa boma hilo Juju-wa-maajuju wakabaki nyuma yake wakipambana wenyewe kwa wenyewe, na wengine wakasalimika na shari yao. Ikifika Siku ya Kiyama likapulizwa baragumu Mwenyezi Mungu atawakusanya viumbe wote kwa ajili ya hisabu na malipo.
Na hayo ni kwa kuwa macho yao walipo kuwa duniani yalikuwa yameghafilika hayaoni Ishara za Mwenyezi Mungu kama kwamba yamezibwa na pazia; na walikuwa kwa upotovu wao hawawezi kusikia Wito wa Haki, kama mtu aliye kuwa kiziwi. "Wale ambao kwamba macho yao yalikuwa paziani hayanikumbuki, na wakawa hawawezi kusikia": Ni wale ambao macho yao yameghafilika na kunizingatia Mimi katika mbingu na ardhi. Na kwa hivyo hii Aya tukufu inazindua watu wazingatie yote yalio wazunguka yanayo onyesha Ishara za kuwepo Mwenyezi Mungu.
Je, macho ya makafiri yamepofuka hata wakadhani kwamba kuwafanya watumwa wangu, Malaika na Isa, kuwa ni miungu, wakiwaabudu badala yangu Mimi, kutawapa manufaa na kuwakinga na adhabu? Hakika Sisi tumewaandalia Jahannamu ndio pahali pao pa kukaa wapate huko malipo wanayo yastahiki.
Ni hao vilio haribika vitendo vyao katika maisha ya duniani kwa kuharibika itikadi yao, na hali wao wanaitakidi kuwa ndio wanafanya vitendo vyema!
Hao ndio walio zikataa dalili za uwezo wa Mwenyezi Mungu, na wakaikanusha Siku ya kufufuliwa na kuhisabiwa. Basi vitendo vyao vimepotea bure, na Siku ya Kiyama watastahiki kudharauliwa na kupuuzwa, kwani hawana a'mali ya kutiwa maanani!
Hayo ndiyo tuliyo yabainisha na tukayapambanua, hali ya hawa; na malipo yao kwa hayo ni Jahannamu kwa sababu ya kufuru zao na kuzifanyia maskhara Ishara za Mwenyezi Mungu alizo ziteremsha, na Mitume alio watuma.
Hakika walio thibiti katika Imani na wakatenda mema, malipo yao ni Bustani za Firdausi watazo ziingia.
Ewe Mtume! Waambie watu: Hakika ujuzi wa Mwenyezi Mungu umekusanya kila kitu. Na lau kuwa maji ya baharini ni wino wa kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu yanayo onyesha ujuzi wake na hikima yake, basi wino huo ungeli malizika, na hata ungeli ongezwa wino mwingine kama huo, kabla ya kumalizika maneno ya Mwenyezi Mungu!
Ewe Mtume! Waambie watu: Hakika mimi ni mtu tu kama nyinyi, nimetumwa kwenu, nikufunzeni aliyo nifunza Mwenyezi Mungu. Nimefunuliwa (yaani nimepewa Wahyi) ya kwamba Mungu wenu ni Mmoja, hana mshirika wake. Anaye tumai kukutana na Mwenyezi Mungu na kupata malipwa yake, basi naatende vitendo vyema kwa usafi wa niya, na ajitenge mbali na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote katika ibada.