"Alif Mym Ra" hizi ni harufi za kutamkwa zimeanzia baadhi ya Sura za Qur'ani. Nazo zinaashiria kuwa huu ni muujiza juu ya kuwa ni harufi wanazo zitumia Waarabu katika maneno yao ya kawaida! Na harufi hizi zilikuwa zikitamkwa huwavutia Waarabu waisikilize Qur'ani! Kwani wale mapagani (washirikina) waliambizana wasiisikilize hii Qur'ani. Ikawa Waumini wakianzia harufi hizi huvutia masikio ya washirikina wakawa wanasikiliza. Hakika hizo Aya au Ishara tukufu ndio hii Qur'ani, Kitabu chenye shani kubwa, uliyo teremshiwa wewe Nabii kwa haki na ukweli kutokana na Mwenyezi Mungu, aliye kuumba, na akakuteuwa. Lakini wengi wa washirikina walio yakanya yaliyo kuja ya Haki si watu wa kuikubali Haki. Bali wao wanaipinga kwa inda.
Hakika aliye kiteremsha hichi Kitabu ni Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye aliye zinyanyua hizi mbingu mnazo ziona zenye nyota zipitazo bila ya nguzo mnazo ziona, wala hazijui mtu ila Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa amezifunganisha hizo na ardhi kwa funganisho zisio katika ila akipenda Mwenyezi Mungu. Na amedhalilisha jua na mwezi chini ya Ufalme wake na kwa ajili ya manufaa yenu. Na jua na mwezi yanazunguka kwa mpango maalumu kwa muda alio ukadiria Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la. Na Yeye Subhanahu anapanga kila kitu katika mbingu na ardhi, na anakubainishieni Ishara zake za kuumba kwa kutaraji mpate kuamini kuwa Yeye ni Mmoja wa pekee.
Na Subhanahu, Mwenyezi Mungu Aliye takasika, ndiye aliye kukunjulieni ardhi, akaidhalilisha ili muweze kutembea juu yake mashariki na magharibi. Na Yeye akajaalia katika hii ardhi milima iliyo simama imara, na mito ya maji matamu inayo miminika. Na akajaalia kwa hayo maji matunda ya kabila mbali mbali yanayo zaliana, na kati ya kabila hizo namna mbali mbali, mengine matamu na mengine makali, mengine meupe, na mengine meusi. Na Yeye Subhanahu huufunika mchana kwa usiku. Na hakika katika huu ulimwengu na ajabu zake zimo alama wazi za kuthibitisha uwezo wa Mwenyezi Mungu na Umoja wake kwa anaye fikiri akazingatia. Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia katika kila mimea dume na jike ili ipate kupandishika sehemu ya uke kwa chembe za uzazi zilioko katika sehemu za ume. Na kwa hivyo ndio huzalikana namna kwa namna na kwa wingi.
Na hakika hiyo ardhi nafsi yake ina maajabu. Ndani yake vipo vipande vilivyo karibiana, navyo juu ya hivyo vina udongo mbali mbali. Vingine ardhi yaabisi, na vingine vya rutba, ijapo kuwa ni udongo ule ule. Ndani yake yapo mabustani yaliyo jaa miti ya mizabibu, na ndani yake mazao mengine yanavunwa, na mitende yenye kuzaa, nayo ama iliyo kusanyika au iko mbali mbali. Na yote hayo ijapo kuwa inanyweshwa maji yale yale yanakhitalifiana kwa utamu wao. Na hakika katika ajabu hizi zipo dalili wazi za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye akili ya kufikiria. Aya hii tukufu inaonyesha ilimu ya ardhi (Geology) na ilimu ya mazingira (Ecology) na athari yao juu ya sifa za mimea. Inajuulikana katika ilimu kuwa rutuba ya ardhi inategemea juu ya chembe chembe za maadeni zinazo khitalifiana kwa namna na ukubwa, na maji yanayo toka kwenye mvua, na hewa, na vitu vyenye asili ya uhai, kama mimea na vyenginevyo, ambavyo hupatikana juu ya udongo au ndani yake. Huwapo hivyo kwa mamilioni vidogo vidogo hata havionekani kwa jicho tu. Kwa jumla ukizingatia haya utaona yanaonyesha uwezo wa Muumba na busara ya uumbaji, kwani ardhi kama wasemavyo wakulimu inakhitalifiana kila shubiri. Na inajuulikana kwa wanazuoni wa sayansi kuwa ukipatikana upungufu katika hivyo vitu vya msingi katika udongo basi hudhihirisha upungufu wake katika mimea, na kwa hivyo wakulima hujalizia upungufu huo kwa kutia mbolea mbali mbali na hutengeneza hali ya mazingira. Na hayo yana athari zake juu ya mazao ikiwa kwa mmea wa namna moja au namna mbali. Ametakasika Mwenyezi Mungu ambaye katika mikono yake upo ufalme wa kila kitu, naye ni Muweza wa kila kitu.
Na hakika mambo ya washirikina juu ya dalili hizi ni ya ajabu. Ikiwa wewe Muhammad utas- taajabia jambo, basi la ajabu ni hiyo kauli yao wanapo sema: Ati baada ya kufa, na baada ya kwisha kuwa mchanga, tutakuwa wahai tena upya? Huu ndio mtindo wa wanao mkufuru Muumba wao. Akili zao zimefungwa na upotovu. Na marejeo yao ni Motoni watakapo dumu humo; kwani hao ni wenye kukanya juu ya kuwa mwenye kuweza kuanzisha anaweza kurejesha.