Mwenyezi Mungu aliye takasika na kila ambalo lisio laiki naye. Yeye ndiye aliye mchukua mja wake Muhammad wakati wa usiku kutoka Msikiti Mtakatifu wa Makka kwendea Msikiti wa Mbali wa Baitul Muqaddas, ambao tuliwabarikia wakaazi majirani wa Msikiti huo katika mahitaji yao, ili tumwonyeshe baadhi ya Ishara zetu zenye ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kuwa Mimi ni Mungu Mmoja peke yangu, na ukubwa wa uwezo wangu! Hakika Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
Na hakika hiyo Baitul Muqaddas ilikuwa inakaliwa na Wana wa Israili baada ya Musa, mpaka walipo fanya fisadi yao humo, wakafukuzwa hapo zamani. Haya ijapo kuwa Sisi tulimpa Musa Taurati, na tukatia ndani yake uwongofu, na tukawaambia: Msimfanye yeyote wa kumtegemezea mambo yenu isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
Nyinyi Wana wa Israili mmezalikana kutokana na wale watu safi wema walio kuwa na Nuhu katika safina baada ya kuwa wameamini. Nasi tukawaokoa wasizame. Basi mfanyeni Nuhu kuwa ndiye mwongozi wenu wa kumfuata, kama walivyo mfanya wazee wenu walio tangulia. Kwani hakika yeye alikuwa mja wa wingi wa shukrani kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake.
Na tukatekeleza hukumu yetu kwa Wana wa Israili katika tuliyo yaandika katika Lauhun Mahfuudh, Ubao Ulio Hifadhiwa, ya kwamba watafanya ufisadi katika Nyumba Takatifu (Baitul Muqaddas) bila ya shaka yoyote mara mbili. Kila mara katika hizo itakuwa ni udhaalimu na uasi, na kuacha hukumu za Taurati, na kuwauwa Manabii, na mtasaidiana katika madhambi, na kwamba utawala wenu utaenea, na kutukuka na kupanda kichwa na kiburi kwa dhulma zenu.
Na ulipo fika wakati wa kukuleteeni adhabu mara ya kwanza, tulikupatilizeni, kwa sababu ya fisadi yenu, kwa kukusalitishieni watu wa kali kupigana. Wakakuingilieni mpaka ndani ya majumba, hapana walicho kiacha, ili wakuuweni. Na ahadi ya kukuadhibuni ilikuwa ni ahadi haina budi kutimizwa.
Kisha mambo yenu yalipo kaa sawa, na mkaongoka, na mkatengeneza umoja wenu, na mkaacha ufisadi, tukakurejezeeni ushindi juu ya wale makhasimu zenu. Nasi tukakuruzukuni mali na wana, na mkazidi kuwa wingi kwa idadi.
Na tukawambia: Mkifanya wema na mkamt'ii Mwenyezi Mungu, wema wenu utakufaeni nafsi zenu duniani na Akhera. Na mkifanya uovu kwa maasi, basi mnajiharibia nafsi zenu vile vile. Na utapo kuja wakati wa adhabu pale mara ya mwisho katika zile mara mbili za ufisadi wenu katika nchi, tutakupelekeeni maadui zenu, wafanye athari za uovu na madhila na huzuni zidhihiri nyusoni mwenu. Na matokeo yake ni kuingia katika Msikiti wa Baitul Muqaddas, wakauharibu kama walivyo ingia na wakauharibu mara ya kwanza, wakateketeza watacho kipata kwa uteketezi mkubwa.