Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanajitoa katika dhima, wala jukumu lolote, na wale washirikina mlio peana nao ahadi, na wao wakavunja hayo mlio ahidiana nao.
Basi nyinyi washirikina, mna amani kwa muda wa miezi mine, kuanzia tangazo hili, mzunguke mtakako katika muda huu. Lakini jueni kuwa popote mlipo nyinyi mko chini ya utawala wa Mwenyezi Mungu, na nyinyi hamuwezi kumshinda Yeye. Na mjue kuwa Mwenyezi Mungu amewaandikia hizaya iwapate hao wanao pinga.
Na hili ni Tangazo linalo toka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuwatangazia watu wote wanapo jumuika siku ya Hija Kubwa ya kwamba:- Hakika Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanajitoa katika dhima, au jukumu, yoyote katika mapatano na washirikina walio fanya khiana. Basi enyi washirikina, mlio vunja ahadi! Mkirudi mkaacha kumshirikisha Mwenyezi Mungu, itakuwa kheri kwenu hapa duniani na kesho Akhera. Lakini mkipuuza na mkabakia hivyo hivyo mlivyo, basi jueni kuwa nyinyi mngali chini ya utawala wa Mwenyezi Mungu. Ewe Mtume! Waonye makafiri wote kuwa ipo adhabu kali yenye uchungu.
Ama wale washirikina mlio ahidiana nao na wakatimiza ahadi zao, wala hawakuacha chochote katika hayo, wala hawakumsaidia yeyote dhidi yenu, basi watimizieni ahadi zao mpaka mwisho na mzihishimu...Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wacha-Mungu wenye kutimiza ahadi zao.
Ukimalizika muda wa amani, yaani miezi mine, basi wauweni washirikina walio vunja ahadi katika kila pahala. Na watieni nguvuni, wazungukeni kwa kuwafungia njia, na wavizieni katika kila njia. Wakitubu wakaacha ukafiri wao, na wakafuata hukumu za Uislamu, kwa kushika Swala, na kutoa Zaka, basi nyinyi hamna sababu ya kuwashambulia, kwa kuwa wamekwisha ingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa wa Kusamehe kwa anaye tubu, na Mwenye rehema kunjufu kwa waja wake.
Ewe Mtume! Mmoja wapo katika washirikina ulio amrishwa uwapige vita, akikutaka amani ili apate kusikia wito wako, basi mpe amani mpaka asikie maneno ya Mwenyezi Mungu. Akiingia katika Uislamu basi huyo ni mwenzenu. Na akitoingia mpeleke mpaka afike pahala pa amani kwake. Na haya ya kumpa ulinzi na amani mwenye kuomba ili asikie maneno ya Mwenyezi Mungu ni kwa sababu ya ule ujinga wake wa kutoujua Uislamu ulio kwisha dhihiri, na ile hamu yake ya kutaka kuujua.