Na tukaifanya milima ni vigingi vya ardhi vya kuituliza? Sehemu ya gamba gumu lilio juu ya ardhi linfikilia kiasi ya kilomita 60 unene wake, na inazidi mikunjo, mifimbi, inapanda juu kuwa milima, na huteremka chini kuwa ni vina vya bahari; na hiyo hulingana kwa sababu ya uzito unao patikana kutokana na milima. Na kulingana huko hakuharibiki ila kwa kubugunyika, kwani gamba kavu la ardhi linazuiliwa na milima, kama vigingi vinavyo zuilia khema. (Rejea Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 7 ya Surat Qaf).
Na tukafanya kulala kwenu ni mapumziko ya machofu ya kazi? Kulala usingizi ni kusita nishat'i ya sehemu ya ubongo yenye kutambua na kuwa macho. Yaani gamba la ubongo, au kupunguka nishat'i yake kwa wingi, ukilinganisha na daraja za nishat'i ya sehemu za viungo vilio baki. Na kwa hivyo kunapunguka nguvu na joto la mwili, tena mwili hapo wakati wa usingizi hupata kutua na kupumzika baada ya kuhangaika viungo au akili au vyote viwili. Basi kazi za kimwili zote hupunguka isipo kuwa kazi za kusaga chakula, na kupitisha mkojo katika mafigo, na kutoka majasho katika ngozi, kwani yakisita hayo hupatikana madhara juu ya maisha ya mtu. Ama kuvuta pumzi huko nako hupunguka, na huwa ni kwa ndani zaidi, na huwa kwa kifua zaidi kuliko kwa tumbo. Na mpigo wa mishipa hupungua kasi kwa kunavyo tokana na moyo, na hudhoofika mkazano wa musulo (muscular tension), na kwa hivyo huwa taabu kupata harakati za kinyume. Na yote haya ni ili binaadamu apate kupumzika wakati wa kulala.
Na Sisi tumeliumba jua lenye mwangaza na linalo waka. Makusudio ya Assiraj Alwahhaaj, Taa yenye mwanga na joto, ni Jua. Na hayo kama ilivyo thibiti katika sayansi kuwa daraja ya joto la uso wake inafika daraja 6000. Ama kati yake daraja yake inazidi daraja 30 milioni kwa sababu ya mdidimizo mkubwa unao patikana juu ya madda ziliomo ndani yake. Na jua linatoa nishat'i hizi zifuatazo: 9 katika 100 ya miale ya Ultraviolet rays, 46 katika 100 ya miale ya mwangaza, 45 katika 100 miale ya joto, au Infra red rays. Na kwa hivyo hii Aya tukufu imeliita kuwa ni Taa yenye mwangaza na joto.
Na tumeteremsha kutokana na mawingu yaliyo karibia kunyesha maji yenye kumiminika kwa nguvu. Mvua ndio kitu pekee kinacho toka asli yake maji matamu katika ardhi. Na asli ya mvua ni kukusanyika vijisehemu vya maji yanayo panda kutoka baharini, na maziwa na mito, yakakusanyika kama mawingu na yakageuka chembe za mvua au vipande vya barafu, na khatimaye yakaanguka kwa sura ya mvua au theluji.
Na milima itaondolewa baada ya kung'olewa mwahala mwake, na kuvurugwa, ikawa unaiona kama sura ya milima na hali hiyo ni kifusi tu kilicho rindikwa, kama uonavyo mangati, sarabi, unaona kama sura ya maji nayo si maji.
Mola Mlezi wa mbinguni na duniani na vilio baina yao, ambaye rehema yake imeenea juu ya kila kitu. Hapana yeyote mwenye madaraka ya kusema mbele yake.
Siku atakapo simama Jibrili na Malaika walio teuliwa nao wamenyenyekea, hasemi mmoja wao ila akipewa idhini na Arrahman, Mwingi wa rehema, kuwa aseme, naye atasema lilio sawa tu.
Hiyo ndiyo siku isiyo na shaka. Basi atakaye na ashike njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi arejee kwa Imani, na a'mali njema.
Hakika Sisi tumekuhadharisheni na adhabu itakayo tokea karibu, siku atakapo angalia mtu vitendo vyake vilivyo tangulizwa na mikono yake, na atakapo sema kafiri kwa kutamani kuokoka: Laiti ningeli bakia udongo baada ya kufa, nisifufuliwe wala nisihisabiwe!