Na lau kuwa Watu wa Kitabu, yaani Mayahudi na Wakristo, wangeli uamini Uislamu na Nabii wake, na wakaacha madhambi tuliyo yataja, tungeli wafutia makosa yao, na tungeli watia katika Bustani (Pepo) za neema, wakastarehe humo.
Na lau kuwa wao wamezihifadhi Taurati na Injili kama zilivyo teremshwa, na wakazitenda, na wakaamini yote waliyo teremshiwa kutokana na Mola wao Mlezi, nayo ni Qur'ani, Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki ikiwajia kutoka kila upande. Na wao si wote sawa katika upotovu. Miongoni mwao, wapo jamaa walio waadilifu, wana akili zao timamu. Hao ndio wale walio muamini Muhammad na wakaiamini Qur'ani. Lakini wengi wao wanatenda vitendo viovu, na wanasema mabaya, na wanajitenga na haki.
Ewe uliye tumwa na Mwenyezi Mungu! Waeleze watu yote uliyo funuliwa na Mola wako Mlezi, na waite wafuate huo ujumbe, wala usiogope maudhi ya yeyote. Na ukitofanya hivyo basi imekuwa hukufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Kwani wewe umekalifishwa ufikishe ujumbe kwa watu wote. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na maudhi ya makafiri. Ni mtindo wake Mwenyezi Mungu kuwa hamnusuru aliye potea akaiacha Haki. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi makafiri kwenye Njia iliyo kaa sawa.
Ewe Mtume! Waambie Watu wa Kitabu (yaani Biblia): Hakika nyinyi hamtakuwa mnafuata Dini sahihi ila mtapo zitangaza hukumu zote za Taurati na Injili na mkazitenda. Na mkaiamini Qur'ani iliyo teremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kwa ajili ya kuwaongoa watu. Na yakinika, ewe Mtume, kwamba wengi wa Watu wa Kitabu watazidi udhalimu, na ukafiri, na inadi, juu ya Qur'ani kwa uhasidi wao na chuki. Basi usiwahuzunikie watu ambao wametiwa muhuri wa upinzani.
Hakika walio muamini Mwenyezi Mungu (yaani Waislamu), na wafwasi wa Musa katika Mayahudi, na walio toka kwenye dini nyenginezo, na wafwasi wa Isa katika Manasara - wote hao wakisafisha imani yao kwa Mwenyezi Mungu, na wakaamini kufufuliwa na malipo na wakatenda mema kama ilivyo funzwa na Uislamu, hao wote watasalimika na adhabu na watakuwa katika furaha ya Peponi Siku ya Kiyama.
Sisi tuliagana na Mayahudi, Wana wa Israili, kwa agano madhubuti katika Taurati kuwa wafuate hukumu zake. Na tukawapelekea Manabii wengi wawabainishie, na wawatilie mkazo ahadi yetu. Lakini walivunja ahadi.Wakawa kila akiwajia Mtume ambaye hakuwafikiana na matamanio yao, ama walimkanusha au walimuuwa.