Na tuliyo kuletea Wahyi wewe katika hii Qur'ani ni Haki tupu isiyo kuwa na shaka yoyote. Tumeiteremsha kuthibitisha Vitabu vilivyo teremshwa kwa Mitume walio kuwa kabla yako, kwa kuwa vyote ni asli moja. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa kujua na kuona kwa waja wake.
Tena tumekifanya Kitabu hichi ni mirathi ya kurithiwa na waja wetu tulio wateuwa. Basi kati yao yupo aliye jidhulumu nafsi yake kwa kuzidi maovu yake kuliko mema yake; na yupo wa kiasi, hakupita mpaka katika maovu yake na wala hakukithirisha mema yake; na miongoni mwao yupo aliye washinda wenginewe kwa kufanya mambo ya kheri, kwa kusahilishiwa na Mwenyezi Mungu. Huko kushinda katika mambo ya kheri ndio kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Malipo yao Akhera ni Mabustani ya daima watayo yaingia. Humo watajipamba kwa vikuku vya dhahabu na lulu. Na nguo zao za Peponi ni hariri.
Na watasema wakisha ingia: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu aliye tuondolea ya kutuhuzunisha. Hakika Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa maghfira, Mwingi wa shukra.
Aliye tuweka kwenye Nyumba ya neema ya milele kwa fadhila zake hatupi taabu humo, wala hatuletei machofu.
Na walio kufuru malipo yao waliyo ahidiwa ni Moto wa Jahannamu watakao uingia. Mwenyezi Mungu hatawahukumia mauti wakafa, wala hawatapunguziwa chembe ya adhabu wakapumzika. Ni kama hivyo tunavyo mlipa kila mwenye kuendelea katika ukafiri na akaushikilia.
Na humo watapiga makelele kuomba msaada wakisema: Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni, tupate kutenda mema siyo yale tuliyo kuwa tukiyatenda duniani. Atawaambia: Hatukukupeni fursa ya kufanya a'mali, tukaufanya mrefu umri wenu kwa muda unao mkinika mtu ndani yake kuzingatia kwa mwenye kuzingatia? Na akukujieni Mtume akakuhadharisheni na adhabu hii. Basi onjeni katika Jahannamu malipo ya udhalimu wenu. Kwani mwenye kudhulumu hapati wa kumnusuru wala kumsaidia.
Hakika Mwenyezi Mungu anajua vyema kila kilicho fichikana katika mbingu na ardhi. Hapana chenye kufichikana kwake. Na lau ange kukubalieni akakurudisheni duniani mngeli rejea yale yale aliyo kukatazeni. Hakika Yeye Mtukufu anavijua vyema vishawishi na vivutio viliomo ndani ya vifua.