Akasema aliye pewa nguvu za kiroho, na ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kiti cha enzi kabla jicho lako halijapepesa. Na akatimiza aliyo yasema. Sulaiman alipo kiona kiti kile kimetua mbele yake bila ya mtingisiko, alisema: Haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu aliye niumba na akanipa kheri zake ili anifanyie mtihani, nitashukuru kwa neema hizi au sitoi haki yake? Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu basi huyo hakika amejiondolea nafsi yake mzigo wa waajibu. Na mwenye kuacha kushukuru kwa neema basi hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi, si mwenye kuhitajia shukrani. Naye ni Karimu wa kuneemesha.