Na tuliwapelekea Thamud ndugu yao Swaleh kuwafunza wamuamini Mwenyezi Mungu pekee. Wao wakakimbilia kugombana na kukhitalifiana. Wakawa makundi mawili. Moja lenye kuamini, na moja la kikafiri.
Swaleh akasema nao kuwanasihi: Enyi watu! Mbona mnaihimiza adhabu mlio ahidiwa kabla ya kutubu? Kwa nini hamwombi msamaha kwa Mola wenu Mlezi, mkamuamini Yeye kwa kutaraji akurehemuni?
Wakasema: Sisi tunakuona wewe na hao walio nawe ni wakorofi, ndio tukapatilizwa na ukame. Yeye akasema: Sababu za kheri na shari zinazo kuteremkieni bila ya shaka yoyote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Bali nyinyi ni watu mnao pewa mitihani ya neema na nakama, ili mpate kuamini.
Na waongozi wa shari kati yao walikuwa ni tisa, kazi yao ni kufisidi katika nchi kwa maoni yao na madai yao. Wala haukuwa mtindo wao kutenda jema lolote.
Wale washirikina wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Apishaneni kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwamba kwa yakini tutamshambulia yeye na ahali zake, na tutawauwa. Kisha tutamwambia jamaa yao wa damu kwamba sisi hatukayaona mauwaji yake wala ya ahali zake. Na hakika sisi ni wasema kweli kwa haya tuliyo yataja.
Walipanga kumuuwa Swaleh na ahali zake, na Mwenyezi Mungu nyuma yao kapanga kumwokoa Nabii wake na ahali zake, na kuwateketeza wao, na hali wao hata hawatambui.
Ewe Nabii! Hebu tazama vipi yalikuwa matokeo ya mipango yao na mipango yetu. Sisi tuliwaangamiza wote hao wao na kaumu yao.
Na hebu yatazame mabaki yao. Utakuta nyumba zao zimeanguka, zimevurugika, kwa sababu ya udhalimu wao na kufru zao, na kumtakia shari Nabii wao. Hakika kwa walio fanyiwa kina Thamud ipo Ishara kwa watu wanao ujua uwezo wetu na wakawaidhika.
Ewe Nabii! Mtaje Luut'i na khabari zake pamoja na kaumu ya watendao uchafu, pale alipo waambia: Je! Mnafanya dhambi hizi ambazo zimepita hadi ya uchafu na kinyume na maumbile, na hali nyinyi mnaona na mnaangalia uovu wa haya mliyo yashikilia?
Hivyo inaelekea katika nadhari ya akili zenu na maumbile kuwaingilia wanaume kwa matamanio yenu, na mkwawacha wanawake? Ama kweli nyinyi mmesibiwa na upumbavu na ujinga wa kufudikiza, hata imekuwa hamwezi tena kuteuwa baina ya kiovu na chema.