Na Waumini walio tangulia kusilimu, na Wahajiri (walio hama Makka kwenda Madina) na Ansari (wasaidizi wa Madina walio wapokea) walio kwenda mwendo mzuri wala hawakufanya taksiri, Mwenyezi Mungu yu radhi nao. Basi anawapokea na anawalipa mema. Na wao kadhaalika wameridhika na wamefurahia aliyo waandalia Mwenyezi Mungu, nayo ni Mabustani yapitayo mito kati ya miti yake. Wataneemeka humo kwa neema ya milele. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
Na katika walio kuwa jirani na Madina miongoni mwa watu wa majangwani, walikuwako walio kuwa wakificha ukafiri wao na wakijidhihirisha kuwa ni Waumini. Na katika wakaazi wa Madina walikuwapo walio kuwa wamezoea unaafiki hata wakawa mabingwa, na wakawa wanauficha watu wasiutambue! Hata mwisho wewe, Mtume, usiwajue. Lakini Mwenyezi Mungu anajua hakika yao, na atawaadhibu duniani mara mbili - mara ya kwanza kwa kuwashinda maadui zenu, na hayo yatawaudhi wao; na mara nyingine kwa kuwafedhehi na kuwakashifu unaafiki wao. Tena, basi, watarejeshwa Siku ya Akhera kwenye adhabu ya Moto, na vitisho vyake vikubwa.
Na wapo watu wengine walio kuudhini, kisha baadae wakakubali makosa yao, na wakafuata Njia ya Haki. Basi watu hao wamefanya vitendo vyema na vitendo viovu. Kwa hao inatarajiwa kukubaliwa toba yao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemu waja wake; huikubali toba yao na huwasamehe.
Ewe Mtume! Pokea kwa hawa wenye kutubu sadaka zao, uwasafishe kwa hizo sadaka makosa yao na uchoyo wao, na unyanyue daraja zao mbele ya Mwenyezi Mungu. Na waombee kheri na uwongofu; kwani kuomba kwako kutawapoza nafsi zao, na zitatulia nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maombi, Mwenye kuwajua wenye nyoyo safi katika toba zao.
Hebu na wajue hao wanao tubu kuwa hakika Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anaye kubali toba ya kweli, na sadaka iliyo safi, na kwamba Yeye Subhanahu ndiye Mkunjufu wa fadhila katika kukubali toba, Mkuu katika kuwarehemu waja wake.
Ewe Mtume! Waambie watu: Tendeni wala msifanye taksiri katika vitendo vya kheri na kutekeleza waajibu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu vyote. Na Mtume na Waumini nao pia wataviona na watavipima kwa vipimo vya Imani, na wataviona kwa mujibu wa itakikanavyo. Kisha mtarudishwa baada ya kufa kwa Mwenye kuijua siri yenu na dhaahiri yenu, apate kukulipeni kwa vitendo vyenu, baada ya kukwambieni dogo lake na kubwa lake.
Na wapo watu wengine wametumbukia katika madhambi - wameacha kwenda kwenye Jihadi, lakini hawana unaafiki. Watu hawa wanangojea amri ya Mwenyezi Mungu. Ama awaadhibu au awakubalie toba yao awasamehe. Na Mwenyezi Mungu anazijua hali zao, na yaliyomo ndani ya nyoyo zao. Naye ni Mwenye hikima kwa ayafanyayo kwa waja wake, ikiwa kuwalipa thawabu au adhabu.