Enyi Waumini! Jilazimisheni kutimiza ahadi zote baina yenu na Mwenyezi Mungu, na ahadi za kisharia zilio baina yenu na watu wengineo. Na Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni kula nyama howa, yaani nyama wa kufuga, kama ngamia, ng'ombe, kondoo, mbuzi n.k. ila wale mlio tajiwa kuwa ni haramu. Wala haikujuzieni kuwinda barani pale mnapo kuwa mmeharimia Hija, au mpo katika eneo la ardhi takatifu. Hakika Mwenyezi Mungu huhukumu apendavyo kwa hikima yake. Yeye ndiye Muumbaji, na ndiye Mwenye kujua jema na baya la viumbe vyake. Na haya ni miongoni mwa ahadi za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu.
Enyi Waumini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Mwenyezi Mungu, yaani ibada alizo amrisha Mwenyezi Mungu, kama ibada za Hija wakati wa Ihram, na sharia na hukumu nyenginezo. Wala msivunje hishima ya miezi mitakatifu kwa kuzua vita katika miezi hiyo. Wala msipinge wanyama wanao pelekwa Makka, kwa kupokonya au kuzuia wasifike huko, wala msiwavue vigwe walivyo fungwa shingoni mwao kuwa ni alama kuwa wamekusudiwa kupelekwa Nyumba Takatifu, na kuwa watakuwa dhabihu wa Hija. Wala msiwapinge wanao kusudia kwenda Hija nao wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Na mkisha vua Ihram na mkatoka kwenye eneo la Alharam, basi mnaweza kuwinda mtakavyo. Wala msipelekewe na chuki yenu kubwa kwa wale walio kuzuieni kufika kwenye Msikiti wa Makka mkawafanyia uadui. Enyi Waumini! Saidianeni katika kutenda kheri na mambo yote ya ut'iifu, wala msisaidiane katika maasi, na kupindukia mipaka aliyo iweka Mwenyezi Mungu. Na ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na nguvu zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuwaadhibu wale wanao mkosa. Mwenye kuhiji akisha "harimiya" (yaani kunuia kuhiji) huwa haramu kwake baadhi ya mambo, kama kuvaa nguo iliyo shonwa, kukata nywele, kuwinda, n.k. mpaka amalize "Ihram" nako ndio kwisha ibada ya Hija.