Ewe Mtume! Hakika Mola wako Mlezi atawapambanua watu wote Siku ya Kiyama kwa uadilifu wake. Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, basi hapana wa kuipinga hukumu yake. Yeye ni Mjuzi wa kila kitu, basi mbele yake kweli haiwezi kuchanganyika na uwongo.
Basi, ewe Mtume, mtegemezee mambo yako Mwenyezi Mungu, na shikilia wito wako kwa kuamini kuwa utashinda tu, kwa sababu wewe uko juu ya Haki iliyo wazi, na mapuuza ya makafiri kukupuuza wewe hakutakudhuru kitu.
Ewe Mtume! Hakika wewe huwezi kuwaongoa hao, kwani hao ni kama maiti kwa kuto tambua kitu, na kama viziwi kwa kutosikia. Basi hao hawako tayari kuusikia wito wako kwa vile walivyo shikilia kukupuuza.
Na wala huwezi kuwaongoa kwenye Haki wale ambao wamepofuka kuona kwao na kutambua kwao. Na huwezi kumfanya asikie ila mwenye kukubali kuziamini Ishara zetu. Hao ndio wenye kut'ii na wenye kuitikia.
Na itapo karibia kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu kuileta Saa ya Kiyama na kuwateremshia makafiri adhabu, Mwenyezi Mungu atawatolea watu mnyama kwenye ardhi atakaye waambia miongoni mwa atakayo sema: Hakika makafiri walikuwa hawaiamini miujiza yetu yote, na pia Siku ya Mwisho. Na hayo waliyo kuwa wakiyakanusha sasa yamekwisha kuwa. Na hichi basi kitisho cha hiyo Saa na yanayo fuatia! Hii ndio tafsiri ya Aya hii kwa dhaahiri ya matamko yake. Na zipo tafsiri mbili nyengine ambazo za hii Aya zinazo weza kuwa: Kwanza ni kuwa makusudio ya "Dabbah" ni yeyote aendaye "yadibbu", katika watu au wengineo. Na hapa inachukuliwa kuwa ni watu, watao kuja kabla ya Kiyama. Na maana yake ni kuwa ikiwateremkia kauli juu yao na adhabu ikathibiti watakuja makundi ya Waumini wakiwaendea, wakienea kote kote, wakizitikisa nguzo za ukafiri. Tafsiri ya pili neno hilo "Dabbah" makusudio yake ni watu waovu, ambao kwa ujinga ni kama wanyama, kama alivyo sema Al As'fahan katika Muqarrarat yake. Na maana yake ni kuwa ikikaribia Siku ya Kiyama, uovu na ufisadi utazidi, na Kiyama wanacho kikanusha makafiri ndio kitakuja. Na hiyo kauli itakuwa, nayo si kauli ya kutamkwa kwa mdomo, lakini kwa kuwa hali yenyewe itakuwa hivyo ni kama iliyo semwa, kama maoni yaliyo kwisha tangulia.
Na ewe Mtume! Kumbuka siku tutapo wakusanya kutoka kila kundi la wenye kukadhibisha Ishara zetu, nao ni hao waongozi wanao fuatwa. Basi hao watachungwa wawe mbele ya kaumu zao kuendea hisabu na malipo.
Na pale watakapo simama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu, atasema Subhanahu kuwaambia kwa kuwadhili na kuwabinya: Nyinyi mlizikadhibisha Ishara zangu zote, na mkazikataa bila ya kuzingatia wala kufahamu. Na khasa mlikuwa mkitenda nini nanyi hamkuumbwa kwa upuuzi?
Bila ya shaka wameshuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameufanya usiku ili wapate kupumzika, na akaufanya mchana una mwangaza, wapate kushughulikia kutafuta maisha yao. Hakika katika hayo zipo dalili wazi za Ungu wa Mwenyezi Mungu, na Upweke wake, kwa watu wanao zingatia wakaamini.
Na taja, ewe Mtume, Siku atapo puliza Israfil baragumu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na watapo ingiwa kiwewe walioko katika mbingu na katika ardhi kwa kitisho cha mpulizo huo, isipo kuwa huyo ambaye Mwenyezi Mungu atamtuliza na akamhifadhi na kitisho. Na viumbe vyote watakuja kwa Mola wao Mlezi nao ni madhalili.
Na unaiona, ewe Mtume, milima na unadhani haitaharaki imetulia tu, lakini kwa hakika inakwenda mbio kama mawingu. Na haya ni katika uundaji wa Mwenyezi Mungu aliye umba kila kitu na akakizua. Hakika Yeye, Subhanahu, ni Mwenye kutimia ujuzi wake kwa yote wayatendayo watu, ya ut'iifu na maasi. Naye atawalipa kwayo. "Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo." Aya hii inathibitisha kuwa vitu vyote vinavyo fuata mvutano wa ardhi, kama milima, bahari, na funiko la anga n.k. vinashirikiana na dunia katika mzunguko wake wa kila siku juu ya msumari-kati wake, na mzunguko wake wa kila mwaka kulizunguka jua. Lakini mzunguko huu hauonekani. Ni kama kwenda kwa mawingu angani. Wanao tazama wanayaona, lakini hawasikii sauti yao, wala hawayagusi. Inaonyesha Aya hii tukufu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye tukuka, ameumba ulimwengu na mipango yake ya kuiendeshea. Naye ni Muweza wa kuifanya hii dunia imetulia tu haizunguki juu ya msumari-kati wake, au akaifanya kuzunguka juu ya msumari-kati wake sawa sawa na kuzunguka kwake kulizunguka jua. Na kwa hivyo ingeli kuwa nusu ya dunia imo kizani totoro kwa muda wa miezi sita, na kwa muda wa miezi sita ikawa nusu ya pili imo katika mwangaza moja kwa moja wa mchana. Na haya yangeli pelekea kuharibika mizani ya joto katika dunia yote. Na kwa hivyo uhai ulioko ungeli toweka duniani. Na Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa Taa'la, ndiye aliye panga mpango huu uliopo kwa rehema yake na huruma zake kwa waja wake. Na juu ya kuwa Aristakhoris, mtaalamu wa ilimu ya falaki wa Iskandaria (Alexandria) katika Misri, aliandika (310-230 K.K.) juu ya kuzunguka dunia wenyewe kwa wenyewe, maandishi haya ya kisayansi ya kale yalikuwa hayajawafikia Waarabu wakati wa Mtume Muhammad s.a.w. au kabla yake. Bali wa mwanzo wa kuashiria mambo haya katika wao alikuwa Albiruni katika mwaka 1000 B.K. (Baada ya Kuzaliwa Nabii Isa), baada ya kuingia kufasiriwa vitabu vya ilimu za zamani kwa lugha ya Kiarabu ulio kuweko katika enzi za Banul Abbas. Basi kutokea haya kwa ulimi wa Mtume Muhammad s.a.w. ambaye aliye kuwa hajapata ilimu hiyo, ni dalili kuwa haya yalifunuliwa kwake na Mwenyezi Mungu.