Kisha Mwenyezi Mungu atakubali toba ya amtakaye katika waja wake, na amsamehe dhambi zake, pindi akirejea kwa usafi wa moyo. Na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa wa kusamehe, Mkuvunjufu wa kurehemu.
Enyi Waumini! Washirikina kwa sababu ya ushirikina wao wamejinajisi nafsi zao, nao wamepotea katika itikadi. Msiwaachilie kuingia Msikiti Mtakatifu baada ya mwaka huu (9 Hijra). Mkichelea ufakiri kwa kukatika biashara Mwenyezi Mungu atakupeni badala yake, na atakutoshelezeni kwa fadhila yake akipenda. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua mambo yenu yote, na Mwenye hikima katika mipango yake.
Enyi mlio amini! Wapigeni vita makafiri katika Watu wa Kitabu wasio muamini Mwenyezi Mungu kwa Imani iliyo sawa, wala hawakiri kuwa kuna kufufuliwa na kulipwa, wala hawayashiki aliyo yakataza Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaishiki Dini ya Haki, nayo ni Uislamu. Wapigeni vita mpaka waamini, au watoe Jizya, nao wamenyenyekea na wat'iifu, si wenye kuasi, wasaidie katika kujenga mfuko wa Kiislamu. "Jizya" ni katika kipato muhimu katika madukhuli ya serikali ya Kiislamu. Kodi hii ilikuwa baina ya Dirham 8 na 40. Kila mtu mmoja katika Mayahudi na Wakristo na walio kuwa kama wao akitozwa Dirham 12. Akilazimishwa kulipa mwanamume aliye kwisha baalighi, na mzima wa mwili na akili, na kwa sharti awe na mali ya kuweza kutoa. Wanawake na watoto walisamehewa, na vile vile vizee. Kwa sababu hao hawapigwi vita. Wala hawatozwi vipofu na wasio jiweza, ila wakiwa matajiri. Kadhaalika hawatozwi mafakiri na masikini na watumwa. Wala hawakutakiwa kutoa mamonaki, yaani mapadri wanao jitenga na watu. Na asli ya kutozwa Jizya ni ulinzi wa wasio kuwa Waislamu. Kwa sababu Ahli Lkitaab, Watu wa Biblia, na walio kama wao, hawakulazimishwa kuingia vitani kulinda nchi wala kujilinda nafsi zao. Kwa hivyo ilikuwa ni haki wao watoe kodi kuwa ni badala ya ulinzi na manufaa mengine ya dola wanayo yapata na wanastarehea nayo. Pia ni badala ya wanacho kitoa Waislamu. Kwani Muislamu anatozwa ile khumsi (moja katika tano) ya ngawira, anatozwa Zaka ya mali, na Zaka ya Fitri, na kafara mbali mbali kwa kulipia makosa. Kwa hivyo ikawa hapana budi kuchukuliwa kodi kutokana kwa asiye kuwa Muislamu badala ya yote anayo yatoa Muislamu kwa maslaha ya wote na kwa ajili ya mafakiri wa wasio kuwa Waislamu. Wala haikukusudiwa kutozwa kodi kuwatia unyonge au kuwatia adabu. Kwani hayo hayaambatani na uadilifu wa Uislamu, wala hayakubaliani na makusudio yake mazuri.
Mayahudi wameacha Tawhidi, ya kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja pekee, na wakasema kuwa Uzair ni mwana wa Mungu! (Mayahudi wa Arabuni tu ndio walimfanya Uzair ni mwana wa Mungu.) Na Wakristo nao wakaacha Imani ya Mungu Mmoja vile vile, wakasema: Masihi ni mwana wa Mungu!! Na kauli yao hii ni ya uzushi, wanakariri kwa vinywa vyao, wala hayakuletwa hayo na Kitabu wala Mtume. Wala hawana hoja wala ushahidi wa hayo. Na katika haya wanafanana na maneno ya washirikina walio kuwa kabla yao! Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri hawa, na atawaangamiza! Ama ajabu watu hawa! Vipi wanaipotea Haki nayo ni dhaahiri inaonekana, na wanakwenda kufuata upotovu!! Uzair ndiye Ezra, Kuhani katika ukoo wa Harun. Alitoka Babilonia walipo rejea Mayahudi mara ya pili, baada ya kufa Mtume wa Mwenyezi Mungu Musa, a.s. kwa kiasi ya miaka elfu. Na huyo Uzair akiitwa "Katibu" kwa kuwa alikuwa akiandika Sharia ya Musa. Angalia: Uzair pamoja na Mayahudi wengine walitoka huko Babilonia kwendea Yerusalemu katika mwaka 456 K.K. (Kabla ya Kristo) katika enzi ya Arikhtisna, Mfalme wa Iran baada ya kuteketezwa Yerusalemu na kuunguzwa Baitul Muqaddas na kunajisiwa kwa muda mrefu
Hao Mayahudi na Wakristo wamewafanya makuhani wao na mapadri kuwa ni "Marabi", kama ni miungu, kwa kuwapa madaraka ya kutunga sharia, na kuwa maneno yao ndiyo dini, ijapo kuwa yanakhitalifiana na kauli za Mtume wao. Wanawafuata katika upotovu wao, na wakamuabudu Masihi mwana wa Maryamu! Na Mwenyezi Mungu amewaamrisha katika hivyo hivyo Vitabu vyao kwa ndimi za Mitume wao, kuwa wasimuabudu ila Mungu Mmoja, kwa kuwa Yeye hapana anaye stahiki kuabudiwa kwa mujibu wa hukumu ya sharia na akili ila Mungu Mmoja. Mwenyezi Mungu ametakasika na kushirikishwa katika ibada, uumbaji, na sifa.