Hakika aliye kiteremsha hichi Kitabu ni Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye aliye zinyanyua hizi mbingu mnazo ziona zenye nyota zipitazo bila ya nguzo mnazo ziona, wala hazijui mtu ila Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa amezifunganisha hizo na ardhi kwa funganisho zisio katika ila akipenda Mwenyezi Mungu. Na amedhalilisha jua na mwezi chini ya Ufalme wake na kwa ajili ya manufaa yenu. Na jua na mwezi yanazunguka kwa mpango maalumu kwa muda alio ukadiria Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la. Na Yeye Subhanahu anapanga kila kitu katika mbingu na ardhi, na anakubainishieni Ishara zake za kuumba kwa kutaraji mpate kuamini kuwa Yeye ni Mmoja wa pekee.