Kama tulivyo wapelekea kaumu zilizo kwisha pita Mitume wakawaeleza yaliyo ya Haki, na wakapotea walio potea, na wakaongoka walio ongoka, na tukawapa miujiza ya kuonyesha Utume wao, kadhaalika tumekutuma wewe kwa umma wa Kiarabu na wenginewe, na kabla yao zimekwisha pita kaumu nyengine. Na muujiza wako ni hii Qur'ani uwasomee, uwawekee wazi maana yake na utukufu wake. Na wao wanaikanya rehema ya Mwenyezi Mungu walio pewa kwa kuteremshiwa Qur'ani. Basi ewe Nabii! Waambie: Mwenyezi Mungu ndiye aliye niumba, na anaye nilinda, na anaye nirehemu. Hapana mungu wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Namtegemea Yeye tu, na kwake ndio marejeo yangu na yenu.
Wao wanataka muujiza mwingine usio kuwa huu wa Qur'ani, juu ya ubora wa athari yake, lau kuwa kweli wanaitaka Haki na wanaikubali. Lau kuwa kuna Kitabu cha kusomwa kikaiendesha milima, kikapasua ardhi, au kikawasemeza maiti, basi Kitabu hicho kinge kuwa hii Qur'ani! Lakini watu hawa wana inda tu. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye amri yote katika miujiza na malipo ya hao wakanyao. Na katika hayo ana uwezo kaamili. Ikiwa hao wamo katika hali hii ya inadi, basi je walio it'ii Haki hawajakata tamaa bado na kuamini kwa hawa makafiri, na wakajua kwamba kufuru yao ni kuyakataa matakwa ya Mwenyezi Mungu? Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka waongoke watu wote basi wangeli ongoka! Na hakika uwezo wa Mwenyezi Mungu uko dhaahiri mbele yao. Basi haziachi balaa kali kali za kuwateketeza zikiwasibu, au kuwateremkia karibu yao, mpaka itimie ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo wapa. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu havunji miadi yake.
Na ikiwa hao wanao kanya wamekufanyia kejeli kwa hayo unao waitia na kwa Qur'ani, basi walifanyiwa maskhara vile vile Mitume walio tumwa kabla yako wewe, ewe Nabii. Basi usihuzunike, kwani mimi nawapa muhula tu hawa wanao kanya, kisha nitawatwaa, na hapo itakuwa adhabu kali isiyo wezekana kuelezwa wala kujuulikana hali yake.
Hakika washirikina wamefanya upumbavu katika kukanya kwao, wakamfanyia Mwenyezi Mungu washirika wa kuwaabudu. Kwani ati huyo ambaye ndiye Mwenye kuhifadhi na kuangalia kila nafsi, na kuipimia kwa kuilipa kheri na shari inayo ichuma, atakuwa wa kufananishwa na haya masanamu? Ewe Nabii! Waambie: Yaelezeni yalivyo kweli! Je, hayo masanamu ya hai? Yanaweza kujikinga na madhara? Yakiwa mawe hayanufaishi wala hayadhuru, basi mbona mnajidanganya nafsi zenu kuwa miungu hiyo ndio imemwambia Mwenyezi Mungu hayo ambayo mnadhani kuwa Yeye hayajui ya ardhi hii? Au mnaiweka kwenye cheo cha kuiabudu kwa maneno yanayo toka katika ndimi zenu? Hakika iliyopo ni kuwa watu hawa wamezugwa na mazingatio yao na mawazo yao ya upotovu. Na kwa sababu hiyo wameiacha Njia ya Haki wakabaki wakitanga tanga! Na wenye kupotea kama hao, basi hawana wa kuwaongoa yeyote, kwani wameziachisha nafsi zao Njia ya Uwongofu.
Duniani watapata adhabu kwa kushindwa na kutekwa na kuuliwa, ikiwa Waumini watakwenda katika njia ya Haki. Na hapana shaka adhabu ya Akhera itayo wateremkia ni kali zaidi na ya kudumu zaidi. Hapana wa kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu Mwenye uwezo wa kila kitu.