Nikakukimbieni nilipo khofu kuwa mtakuja niuwa kwa jinaya hii ambayo sikuukusudia. Mola wangu Mlezi akanitunukia fahamu na ilimu, kwa fadhila zake na neema zake, na akanifanya mmoja katika Mitume.
Musa akaashiria sifa katika sifa ovu kabisa za Firauni, nayo ni kuwa kawafanya watumwa Wana wa Israili, na akiwauwa watoto wao wanaume. Na akakataa kukuita kule kulelewa kwake katika jumba la Firauni kuwa ni neema, kwani yaliyo sabibisha hayo ni yale aliyo kwisha yataja, ndio yeye alitupwa mtoni aokoke asiuliwe. Akaishia kwenye jumba la Firauni. Na lau kuwa si hivyo basi angeli lelewa na wazazi wake.
Musa akasema: Yeye huyo ndiye Mwenye kuzimiliki mbingu na ardhi na kila kilio baina yao. Ikiwa nyinyi mna yakini ya ukweli wa jawabu hii basi mtanafiika, na mtaongoka, na mtajua kuwa ufalme wa Firauni wa kujidai haufui dafu mbele ya Ufalme wake Mwenyezi Mungu. Kwani ufalme wa Firauni haupindukii hata eneo moja katika hii dunia.
Firauni kuonyesha mastaajabu kwa wale walio mzunguka kwa kuwa Musa katika jawabu yake alipo mtaja Mola wake Mlezi na akadhukuru Ufalme wake hakuugusia hata kidogo ufalme wa Firauni, alisema: Mwayasikiaje maneno ya Musa?
Musa akiendelea na usemi wake bila ya kujali hasira za Firauni na uchafu wa maneno yake, akasema: Ndiye huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote, aliye kuumbeni nyinyi na baba zenu walio tangulia. Na miongoni mwa hao walikuwako walio dai ungu kama unavyo dai wewe. Na wao wameteketea. Na wewe utateketea, na hayo unayo yadai yatapotelea mbali. Kwani Mungu wa kweli hafi.
Firauni akwaambia watu wake yale yanayo mtibuwa roho na kumghadhibisha, akautaja Utume wa Musa ni kwao wao, wala si kwake yeye, na akambandikiza wazimu, kwa kuwa ati akiulizwa kitu hujibu kingine, na anamsifu Mola Mlezi kwa sifa za kiajabu ajabu. Na kwa hivyo Firauni anawahimiza wamkadhibishe.
Musa akasema: Ikiwa nyinyi mna akili, basi uaminini Ujumbe wangu. Kwani kuchomoza jua na kuchwa kwake kwa mpango madhubuti ni dalili wazi ya Mwenye kuumba. Kwa hivyo basi ni nyinyi ndio mnastahiki kuambiwa wendawazimu.
Firauni akamwambia Musa: Ukimfuata mungu yeyote badala yangu mimi, utakuwa mmoja katika wanao ijua hali yao mbaya katika magereza yangu. Na yeye Firauni kaangukia kitisho hichi baada ya kushindwa kuondoa athari za kazi za Muumbaji.
Firauni akasema: Ulete ushahidi utao onyesha Unabii wako kama wewe kweli unasema kweli katika wito wako. Kasema hayo kwa tamaa ya kuwa huenda akapata kipengee cha udhaifu katika hoja zake.
Firauni akawaambia watu wake: Hakika Musa ni mchawi bingwa katika uchawi wake. Kasema hayo kwa kuchelea watu wake wasiifuate Haki waliyo iona kwa Musa.
Tena Firauni akasema: Mchawi huyu anataka kunifanyia kahari apate kukutoeni katika hii nchi yenu. Na haya ni uchochezi dhidi ya Musa, kwani katika la dhiki mno katika hayo yaliyo dhiki ni mtu kuiacha nchi yake, na khasa ikiwa kwa kahari. Naye akataka mawazo ya wale walio kuwa wanamuabudu. Kasahau ungu wake kwa nguvu za Ishara za Musa.
Watu wake wakamwambia: Akhirisha kukata shauri yao hawa, na uwatume askari wende wawakusanye wachawi katika raia zako. Kwani uchawi hupingwa kwa uchawi.